Michezo

Cech kuwasaidia Arsenal kuchabanga Chelsea kwa mara ya nne katika fainali

May 13th, 2019 2 min read

NA MASHIRIKA

PETR Cech, 36, huenda awe kiini cha kusimama kwa bahati ya Arsenal katika jitihada za kikosi hicho cha kocha Unai Emery kufuzu kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Kipa huyo mzaliwa wa Jamhuri ya Czech atakuwa akiwaongoza Arsenal kuvaana na waajiri wake wa zamani, Chelsea katika fainali nne za vipute vya haiba kubwa. Cech ataangika rasmi glavu zake katika ulingo wa soka mwishoni mwa msimu huu, kumaanisha kwamba mchuano wake wa mwisho kitaaluma utamshuhudia akiyapangua makombora ya ‘The Blues’ jijini Baku, Azerbaijan mnamo Mei 29, 2019.

Hata hivyo, anajivunia rekodi ya kuridhisha sana dhidi ya Chelsea katika fainali za kuwania mataji. Pindi alipobanduka London Magharibi na kutua London Mashariki mnamo 2015, Cech aliwaongoza Arsenal kuwapepeta Chelsea 1-0 katika kivumbi cha kuwania Community Shield uwanjani Wembley.

Miaka miwili baadaye, aliwasaidia Arsenal kufuzu kwa fainali ya Kombe la FA iliyowakutanisha na Chelsea mnamo 2017.

Ingawa Cech alisalia kwenye benchi, mabao kutoka kwa Alexis Sanchez na Aaron Ramsey yaliwasaidia Arsenal kuwazima Chelsea na hivyo kumvunia kocha Arsene Wenger Kombe la FA kwa mara ya saba.Kwa kuwa Chelsea walitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2016-17 chini ya kocha Antonio Conte, ufanisi huo uliwaweka katika ulazima wa kuchuana na Arsenal katika Community Shield wiki 10 baadaye.

Cech alipangwa katika kikosi cha kwanza kwenye kipute hicho kilichokamilika kwa sare ya 1-1 mwishoni mwa dakika 120. Arsenal waliibuka washindi baada ya Thibaut Courtois na Alvaro Morata kupoteza mikwaju yao ya penalti.

Ni matumaini ya mashabiki Arsenal kwamba Cech ambaye amekuwa kipa katika mechi za Europa League, ‘atastaafu vyema’ kwa kuwaongoza kufuzu kwa kampeni za UEFA muhula ujao.

Akizungumza kabla ya Arsenal kurudiana na Valencia katika nusu-fainali nchini Uhispania wiki jana, Cech alikiri kwamba kumenyana na Chelsea katika mchuano wake wa mwisho kitaaluma, kutamfanya mwingi wa hisia jijini Baku.

“Kucheza fainali ya Europa League dhidi ya Chelsea ambao pia ninawastahi sana, huenda kuwe jambo zito zaidi mimi kuhimili,” akatanguliza.Baada ya kufichua azma ya kustaafu, kisha kupangwa dhidi ya Rennes katika droo ya robo-fainali, dalili zote ziliashiria kwamba Arsenal wangekutana na Chelsea katika fainali.”

“Ninaishi karibu sana na uwanja ambao Chelsea hufanyia mazoezi yao jijini London. Watoto wangu husomea shule moja na wa wachezaji wengi wa Chelsea. Isitoshe, mwanangu Damian ni kipa wa Chelsea kwa kikosi cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 10. Ningali katika kundi moja la WhatsApp na masogora wote niliowahi kucheza pamoja nao kambini mwa Chelsea, wakiwemo Didier Drogba, Frank Lampard, John Terry na Ashley Cole.”