CECIL ODONGO: Azma ya Wanjigi ni mbinu ya ODM kupenya Mlima Kenya

CECIL ODONGO: Azma ya Wanjigi ni mbinu ya ODM kupenya Mlima Kenya

Na CECIL ODONGO

TANGAZO la mfanyabiashara tajiri Jimmy Wanjigi kuwa analenga kupigania tiketi ya ODM ili kuwania kiti cha Urais 2022, ni njama fiche ya kuhakikisha Raila Odinga anapata sehemu ya kura milioni sita za eneo hilo.

Bw Wanjigi anaonekana kutotetereka katika kile anachodai ni azma yake ya kuingia ikulu na amekuwa akikariri mara kwa mara kuwa atapigania tiketi ya ODM, akiwa na matumaini ya kumbwaga Bw Odinga.

Mwanzo, Jimmy Wanjigi si mgeni katika siasa za Kenya na inaamika alichangia pakubwa katika kufanikisha ndoa ya kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013.

Baada ya kukosana na wawili hao alielekea upande wa Bw Odinga katika uchaguzi wa 2017 huku akidaiwa kutumia mifuko yake mizito kufadhili kampeni za mwanasiasa huyo anayelenga kuwania Urais kwa mara ya tano.

Hata hivyo, mwenendo wa Bw Wanjigi hasa baada ya kufanya mikutano yake Nakuru na Nyeri na wajumbe wa ODM, akisisitiza yupo mchujoni, inaashiria kuwa huenda nia yake hasa si kuwania Urais ila kumsaidia ‘Baba’ kupenya mlimani.

Pili, ni jambo la wazi kuwa kudai kwamba atapigania tiketi ya ODM na kumshinda Bw Odinga ni jambo ambalo haliwezekani.

Hii ni kwa sababu Bw Odinga ni ODM na chochote chamani hakiwezi kuendelea bila idhini yake wala washirika wake hata hawachukulii kwa uzito azma ya Bw Wanjingi.Kwa hivyo, kwa Bw Wanjigi kudai ana imani kuwa ana uwezo wa kumshinda Bw Odinga mchujoni ni ‘kujifanya’ tu.

Je, atapata wapi wajumbe wa kutosha wa kumpitisha dhidi ya Bw Odinga wakati wa Kongamano Kuu la ODM la kumuidhinisha mwaniaji wa Urais?

Ni vyema kumkumbusha Bw Wanjigi kuwa kuelekea kura ya 2013, Musalia Mudavadi na kundi lake likiongozwa na viongozi kutoka eneo la Magharibi walizuru kaunti kadhaa baada ya Makamu huyo wa Rais kutangaza kuwa atampinga Bw Odinga wakati wa mchujo wa ODM.

Hata hivyo, ilimlazimu, Bw Mudavadi na baadhi ya wanasiasa wandani wake wakiongozwa na Seneta wa Vihiga George Khaniri kuhama ODM na kubuni United Democrati Forum (UDF).

Bw Mudavadi alionekana kuwa na wajumbe wengi waliokuwa wakimuunga mkono dhidi ya Bw Odinga katika ODM, ila mrengo wake ulihisi mapema kuwa hakungekuwa na demokrasia na mchujo huo ungevurugwa.

Mchujo

Vivyo hivyo, mwaka jana Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho, walitangaza kuwa watashindana na Bw Odinga katika mchujo wa ODM. Hata hivyo, wawili hawa sasa wamenywea huku wakivumisha azma ya Bw Odinga wakitumai kupata nyadhifa muhimu akiingia serikalini.

Tayari Bw Odinga anadaiwa kuungwa mkono na wafanyabiashara matajiri kutoka Mlima Kenya ila huenda mbinu anayotumia Bw Wanjigi ni kwanza kufanya uwepo wa ODM angalau uhisiwe mlimani kisha iwe rahisi kuwashawishi wakazi kukumbatia azma ya Bw Odinga.

Pia mikutano yake inalenga kumsongesha Bw Odinga karibu na wakazi wa Mlima Kenya ili aanze kujivumisha kwa kigezo kuwa anasaka uungwaji mkono wa wajumbe wa ODM eneo hilo kushindana na Bw Wanjigi mlimani.

Kwa kuwa eneo hilo huenda lisiwe na mwaniaji maarufu wa Urais jinsi walivyokuwa Mzee Jomo Kenyatta, Kenneth Matiba, Mwai Kibaki na Rais Kenyatta, Bw Odinga anatumai angalau ataongeza kura zake katika eneo hilo ambalo amekuwa akionekana kuwa na uadui mkubwa kisiasa.

You can share this post!

Okutoyi aanza tenisi ya J2 Cairo kwa ushindi

MARY WANGARI: Kenya yahitaji mbinu za kisasa kuboresha...