CECIL ODONGO: Jamii ya Mulembe isake msemaji mwengine baada ya ‘kusalitiwa’

CECIL ODONGO: Jamii ya Mulembe isake msemaji mwengine baada ya ‘kusalitiwa’

NA CECIL ODONGO

BAADA ya kuwa dhahiri kuwa Musalia Mudavadi wa ANC na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya hawatakuwa debeni Agosti 9, wakazi wa uliokuwa mkoa wa Magharibi wanafaa wateue kigogo mpya wa siasa za jamii ya Waluhya kuwaongoza miaka inayokuja.

Licha ya jamii hiyo kuwa na kura nyingi na ndio ya pili kwa idadi ya watu nchini, Mabw Mudavadi na Wetang’ula wamekosa kuonyesha uongozi bora na kutoa mwelekeo.

Mwaka huu wameiponza jamii yao kwa kughairi nia ya kuwania uongozi wa nchi katika uchaguzi mkuu kisha kumuunga mkono Naibu Rais Dkt William Ruto.

Alipokuwa akizundua azma yake ya kuwania kiti cha urais mnamo Januari 2022 katika ukumbi wa Bomas, Bw Mudavadi alisema kuwa mara hii hangeghairi nia na kumuunga mkono mwanasiasa mwengine jinsi alivyofanya 2002, 2007 na 2017.

Katika hotuba yake ambayo ilijaa kauli ‘Tusidanganyane’, Bw Mudavadi alimkashifu kiongozi wa ODM Raila Odinga akimtaja kama mwanasiasa mnafiki ambaye alipuuza mkataba waliokuwa nao ndani ya muungano wa NASA na kuwasaliti vinara wenzake.

Akitangaza kuwa wangejiunga na muungano wa Kenya Kwanza, Bw Mudavadi aliwapa wakazi imani kuwa angepambania tikiti ya kuwania Urais kwenye mchujo pamoja na Naibu Rais Dkt William Ruto katika muungano huo

Hata hivyo, mambo sasa yamemwendea mrama Bw Mudavadi baada ya mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua kuchaguliwa mgombeaji mwenza wa Dkt Ruto.

Sasa Bw Mudavadi amekosa nafasi ya kuwania Urais, kuwa mgombeaji mwenza huku akitegemea ahadi ya kupokezwa wadhifa wa waziri mwenye mamlaka makubwa ambao hata haupo kwenye katiba.

Pamoja na Bw Wetang’ula, wameahidiwa asilimia 30 ya serikali iwapo Dkt Ruto atashinda Urais na kutwaa uongozi wa nchi lakini lazima wahakikishe wakazi wa Magharibi wanapigia UDA kura kwa asilimia 70.

Masharti hayo ni magumu mno kutimizwa ikizingatiwa kwamba Bw Odinga na muungano wa Azimio la Umoja nao wana uungwaji mkono mkubwa katika eneo hilo.

Hata alipowania uongozi wa nchi mnamo 2013, Bw Mudavadi alipata chini ya asilimia 30 za kura za wakazi wa Magharibi.

Kwa kifupi, Mabw Mudavadi na Wetang’ula hawatakuwa na usemi au ushawishi katika serikali ya Dkt Ruto na endapo watapoteza uchaguzi huo basi ndoto zao za kisiasa zitazidi kudidimia zaidi.

Hata wakishinda itabidi wawe wakicheza siasa zao chini ya himaya ya Dkt Ruto ambaye lazima ataongoza kwa mihula yote miwili kabla ya kumpisha kiongozi mwengine.

Baada ya kutawazwa kama msemaji wa jamii hiyo mnamo Disemba 31, 2016 katika hafla iliyoongozwa na Katibu wa Cotu Francis Atwoli, Bw Mudavadi anaonekana amelemewa kuunganisha jamii hiyo huku maamuzi aliyoyafanya kisiasa yakimponza na kumletea shida.

 

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Nchi itanawiri zaidi tukiwapa wanawake nafasi

CHARLES WASONGA: Vyuo vikuu vishirikiane na soko la ajira...

T L