CECIL ODONGO: Kadhi Mkuu mpya sasa atoke eneo jingine la nchi

CECIL ODONGO: Kadhi Mkuu mpya sasa atoke eneo jingine la nchi

Na CECIL ODONGO

WAISLAMU wanafaa wapate Kadhi Mkuu mpya kutoka maeneo mengine nchini isipokuwa Pwani na Kaskazini Mashariki wakati ambapo muhula wa kudumu kwa Sheikh Ahmed Muhdhar utakuwa unakamilika mnamo Novemba mwaka huu.

Japo kuna mchakato wa kisheria unaofuatwa katika kuwapiga msasa wanaoawania wadhifa huo shughuli inayotekelezwa na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC), ni vyema kwamba Waislamu wakubaliane ili mtu anayetoka eneo jingine kando na maeneo hayo mawili apewe wadhifa huo.

Kwa sasa wadhifa wa Kadhi Mkuu unashikiliwa na mtu kutoka Pwani na Naibu wake anatoka Kaskazini Mashariki. Haitaonekana vyema iwapo nyadhifa hizo mbili zitashikiliwa tena na watu kutoka maeneo hayo mawili ilhali kuna viongozi Waislamu waliohitimu kushikilia nafasi hizo kutoka maeneo mengine.

Kadhi wote watano tangu taifa ijinyakulie uhuru, Abdalla Kassim, Swale Abdalla, Nassor Nahdy na Hammad Kassim wametoka Pwani huku manaibu wao wakitokea Kaskazini Mashariki.

Kumteua Kadhi Mkuu kutoka maeneo ambayo hajawahi kushikilia wadhifa huo utawafanya waumini wao wahisi hawajatengwa katika kuendesha masuala ya dini hiyo licha ya kwamba idadi ya waumini si wengi ikilinganishwa na Pwani na Kaskazini Mashariki.

Baadhi ya majukumu ya Kadhi Mkuu ni kuamua kuhusu masuala tata ya ndoa hasa talaka na urithi wa mali. Pia Kadhi Mkuu ana jukumu la kuwaongoza Waislamu katika kuamua siku ambayo waumini wataanza kufunga kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan na kukamilika kwa mfungo huo.

Siku hiyo huafikiwa kutokana na mwaandamo wa mwezi jambo ambalo limekuwa likizua utata hasa kati ya Waislamu wa bara na wale wanaotoka Pwani na maeneo ya Kaskazini Mashariki.

Wengi wa Waislamu wanaotoka bara huanza kufunga au kumaliza mfungo wao kwa kulingana na mwaandamo wa mwezi nchini Saudia wala si amri ya Kadhi Mkuu.

Ni kweli kwamba majukumu ya Kadhi Mkuu ni mazito na yanahitaji umakinifu mkubwa na hekima katika kuyatekeleza lakini hata Waislamu wanaotoka bara wanatosha kuhudumu katika wadhifa huo muhimu.

Aidha kuna mashirika mbalimbali ya Kiislamu ambayo yamekuwa yakiongozwa na Waislamu ambao hawatoki Pwani na Kaskazini Mashariki na yamekuwa yakitekeleza majukumu yake vyema tena kwa usawa kwa Waislamu.

Baraza Kuu la Waislamu (SUPKEM) linaongozwa na Sheikh Hassan Ole Naado ambaye hatoki Pwani au Kaskazini Mashariki. Japo Supkem limekumbwa na misukosuko ya uongozi siku za nyuma, sasa limekuwa dhabiti na limekuwa sauti ya Waislamu kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa.

Aidha viongozi wa kisiasa Waislamu hawafai kuingilia mchakato wa kuteuliwa kwa Kadhi Mkuu ili kumpata mtu ambaye watamdhibiti kwa kuwa hii ni asasi ya kidini na inafaa ihusike na mwelekeo wa dini na wala si siasa.

Uislamu ni dini yenye umoja na unaozingatia usawa kwa hivyo, suala la wadhifa wa Kadhi Mkuu halifai kuzua mgawanyiko miongoni mwa waumini.

You can share this post!

Vitambulisho vya kitaifa kufutiliwa mbali, Huduma Namba...

Messi afunga mawili dhidi ya Huesca na kufikia rekodi ya...