NA CECIL ODONGO
NI kinaya kuwa Kenya inaendesha juhudi za kupatanisha mataifa ambayo yamekita katika mapigano ya kisiasa, ilhali huku kwetu viongozi wanazozana kwa misimamo mkali.
Vigogo wakuu nchini, Rais William Ruto na kinara wa upinzani Raila Odinga, wanaendelea na uhasama kuhusu uchaguzi mkuu uliopita ambao kinara huyo anadai ulijaa udanganyifu.
Kwa wiki ya tatu mfululizo, Bw Odinga anatarajiwa kuongoza mkutano mwingine mkubwa katika mtaa wa Kibera kushinikiza utawala wa Kenya Kwanza uondoke mamlakani.
Waziri Mkuu huyo wa zamani tayari amesema hatambui ushindi wa Rais Ruto na ataendeleza maasi dhidi ya serikali hadi haki ifanyike.
Hili si suala la kupuuza kwa sababu iwapo maandamano yatafanyika kila wiki, italeta picha mbaya na hata kufukuza wawekezaji.
Pia, ikumbukwe kuwa kupanda kwa gharama ya maisha ni kati ya mambo ambayo huenda yakaongezea ghadhabu za raia dhidi ya serikali.
Tatizo letu si dogo ilhali wanasiasa wanalifumbia jicho na kuendelea kupatanisha mirengo inayozozana kule Somalia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta amekuwa akiendesha vikao vya upatanishi kati serikali ya DRC na wapiganiaji wa M23, ambao wapo Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka naye kwa miaka mingi amekuwa akiongoza juhudi za upatanishi kule Sudan Kusini, ambapo Rais Salva Kiir Mayadit na makamu wake Riek Machar hawaonani ana kwa ana.
Kwa kuendesha juhudi hizi za upatanishi, kama taifa tunasema hali ni shwari kwetu.
Rais Ruto na Bw Odinga wanastahili kufuata mfano wao wa patanisho ili waridhiane, badala ya Kenya kuwa na viongozi wanaotuliza joto kule nje ilhali kwetu kumejaa mgawanyiko.
Subscribe our newsletter to stay updated