CECIL ODONGO: Kupe wa kisiasa wataponza Mudavadi na Kalonzo 2022

CECIL ODONGO: Kupe wa kisiasa wataponza Mudavadi na Kalonzo 2022

Na CECIL ODONGO

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi wanafaa wajihadhari na baadhi ya wabunge na maseneta wanaowasukuma wawanie urais ilhali kwa kiasi kikubwa hawana uungwaji mkono wa kutosha wa kuwawezesha kuingia ikulu.

Licha ya kuwa viongozi hao wawili ambao wamewahi kuhudumu kama makamu wa Rais wametangaza kuwa debeni, kwa asilimia kubwa itakuwa vigumu kwao kuingia ikulu wakitegemea tu kura kutoka ngome zao.

Bw Musyoka ana uungwaji mkono wa kupigiwa mfano miongoni mwa jamii ya Wakamba hasa katika kaunti tatu za Kitui, Makueni, Machakos na sehemu ya Pwani.

Kwa upande mwingine, Bw Mudavadi anajikakamua kuunganisha kura za jamii ya Waluhya hasa katika eneo la Magharibi ya nchi.

Wanasiasa hawa wawili hawajivunii uungwaji mkono mkubwa ikilinganishwa na wapinzani wao wakuu Naibu Rais Dkt William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ambao wanaonekana kuwa kifua mbele kwenye kiny’ang’anyiro cha urais.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wabunge na maseneta wandani wa Mabw Musyoka na Mudavadi ambao wanalenga tu kutumia umaarufu wa wanasiasa hao Ukambani na Magharibi mtawalia, kuvishinda viti vya ugavana, Useneta, ubunge au udiwani bila kujali hatima ya vigogo hao 2022.

Kati ya wanasiasa hao ni Seneta wa Kitui Enock Wambua na mwenzake wa Kakamega Cleophas Malala ambao wamekuwa wakishinikiza uwaniaji urais wa wawili hao.

Ingawa si vibaya kwao kuwavumisha Mabw Musyoka na Mudavadi jinsi wanaODM na UDA wanavyoendeleza injili ya Dkt Ruto na Bw Odinga, inaonekana lengo lao kuu ni kutwaa viti vya ugavana.

Vitisho

Bw Wambua kwenye kikao na wanahabari wiki jana alisisitiza kuwa iwapo Bw Musyoka ataunga mkono Bw Odinga, basi yupo tayari kuwaongoza wapigakura Ukambani kumuasi kisiasa.

Seneta huyu analenga ugavana wa Kitui kupitia Wiper dhidi ya mshikilizi wa sasa Charity Ngilu ambaye ametangaza kuwa atatetea kiti chake.

Kwa hivyo, anajitahidi sana aonekane kama anayeshambulia Bw Odinga na kusukuma urais wa Bw Musyoka ili kuvutia kura za ugavana nyumbani bila kujali hatima ya kiongozi huyo wa chama chake.

Vivyo vivyo, Bw Malala amekuwa akikemea sana Bw Odinga tangu arejee kambini mwa Bw Mudavadi akilenga kurithi kiti cha ugavana baada ya Wycliffe Oparanya kutamatisha hatamu yake mwakani.

Katika miaka mitatu yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa, Bw Malala alikuwa na ukuruba na chama cha ODM na alikuwa akihudumu kama Naibu Kiongozi wa wengi licha ya kuchaguliwa kupitia ANC.

Mnamo Juni, 2020 ANC hata iliandikia barua msajili wa vyama vya kisiasa ikiomba jina la Bw Malala liondolewe kama mwanachama wa ANC.

Baada ya kutemwa kutoka uongozi wa seneti na ODM, Bw Malala alirudi ‘nyumbani’ akaomba msamaha na kuanza kampeni za kuvumisha Bw Mudavadi, nia ikiwa kutumia ANC kuwania ugavana.

Na si Mbw Malala na Wambua pekee, bali kuna wengi ambao wananyemelea viti vya ubunge chini ya vivuli cha vinara wa vyama vyao.

You can share this post!

MARY WANGARI: Kongamano la UN litumiwe kuimarisha mifumo ya...

Kituyi akemea Uhuru, amtaja kama dikteta