CECIL ODONGO: Madai ya Ruto, Amerika yanalenga kusawiri Nyanza kama uwanja wa fujo

CECIL ODONGO: Madai ya Ruto, Amerika yanalenga kusawiri Nyanza kama uwanja wa fujo

NA CECIL ODONGO

MADAI ya Naibu Rais, Dkt William Ruto kuwa amezuiwa kuendesha kampeni katika eneo la Luo Nyanza na hatua ya Amerika kuwataka raia wake wasitembelee Kisumu kipindi hiki cha uchaguzi inalenga tu kuwasawiri wakazi wa Nyanza kama wapenda fujo.

Akiwa katika mkutano wa kisiasa Eldoret wiki jana, Dkt Ruto bila kutoa ushahidi, alidai Kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga amemzuia kufanya kampeni katika eneo hilo.

Dkt Ruto hasa alisema, anahofia kushambuliwa, akirejelea kisa cha mwaka 2021 ambapo gari lake lilipigwa mawe Kondole.

Matamshi haya yanashangaza kwa sababu, sheria haimzuii yeyote kuzuru eneo lolote kwa jambo lolote lile.

Kama Naibu Rais, Dkt Ruto ana mamlaka makubwa na hawezi kuzuiwa kufika Kisumu kwa shughuli zozote zile, ziwe za serikali au kwenye kampeni.

Pili, kuna wanasiasa wa UDA ambao wanawania viti mbalimbali eneo la Nyanza na wamekuwa wakifanya kampeni bila kutatizwa na yeyote.

Je, sembuse Dkt Ruto?

Kile kinachoonekana kuhofisha Dkt Ruto kufika Kisumu ni kuwa, alifahamu huenda wakazi wasivumilie matamshi yake ya uchochezi na kuwakebehi Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

Japo wamekuwa wakisawiriwa kama watu wenye ghasia, eneo la Luo Nyanza ndilo lilikuwa kitovu cha vita vya kupigania ukombozi wa pili.

Juhudi zao za kupigania haki na kupinga dhuluma hazifai kufasiriwa kama nia ya kusababisha fujo.

Amerika kuwaonya raia wake ni picha mbaya kwa sababu, hakuna ripoti zozote za kijasusi nchini ambazo zimeonyesha uwezekano wa kuzuka kwa ghasia Kisumu na maeneo ya karibu baada ya matokeo ya uchaguzi wa Jumanne kutangazwa.

Kusawiri tu wakazi wa Kisumu na Luo Nyanza kama wanaohusudu ghasia si vyema.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Kudhulumu wahudumu ni kosa, adhabu yake ni...

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Maulana atujaalie tuwe na uchaguzi wa...

T L