CECIL ODONGO: Matamshi ya Raila kikwazo kwa azma yake kuwa rais

CECIL ODONGO: Matamshi ya Raila kikwazo kwa azma yake kuwa rais

Na CECIL ODONGO

MATAMSHI tata ya Kinara wa ODM Raila Odinga kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa kila mara Uchaguzi Mkuu unapokaribia kwa njia moja au nyingine yamechangia kushindwa kwake kwa kuwa yanatumiwa na wapinzani wake kumpiga vita na kumpungizia umaarufu.

Kiongozi huyu wa ODM ambaye bila shaka ana umaarufu kwa karibu nusu ya wapigakura hapa nchini, anafaa achunge ndimi zake asitoe matamshi ambayo yatatumiwa na wapinzani wake kudidimiza nafasi yake kuingia ikulu mnamo 2022.

Mwishoni mwa wiki jana, Bw Odinga akiwa ziarani Kaunti ya Mombasa alisema kuwa atawafunga viongozi wafisadi atakapochukua hatamu za uongozi iwapo atafanikiwa kuingia serikalini 2022.

Tamko hili limefasiriwa kuwa linalolenga kambi ya Naibu Rais Dkt William Ruto ambao wandani wake wanakabiliwa na madai ya uporaji wa mali ya umma.

Hata Dkt Ruto mwenyewe amekuwa akifasiriwa kama kiongozi fisadi na wafuasi wa Bw Odinga.

Ikizingatiwa kwamba uchaguzi mkuu ujao bado umesalia mwaka moja ufanyike, washauri wa Bw Odinga wanafaa wamwelekeze asiwe akizungumza tu kiholela kuhusu masuala ambayo yanaweza kumpunguzia kura.

Kusema kwamba atawafunga wafisadi nchini kutampunguzia umaarufu kwa kuwa hata baadhi ya viongozi wa ODM ambao wanamuunga mkono wanakabiliwa na mashtaka ya ufisadi.

Kwa hivyo, wanaweza kudai kuwa wanamuunga ila wafanye mipango ya chini kwa chini kusambaratisha azma yake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 ndipo wajiokoe katika mpango wake.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2013, Bw Odinga, akiwa waziri mkuu alikuwa na nafasi nzuri ya kuingia ikulu lakini matamshi yake kuwa viongozi waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya ICC wafungwe yalimchongea.

Kauli hiyo ilirejelea hasa Uhuru Kenyatta (wakati huo akiwa Naibu Waziri Mkuu) na Dkt Ruto wakati huo akiwa waziri wa elimu.

Bw Odinga ambaye alikuwa na matumaini tele alikuwa akipanda jukwaani kila mara na kukashifu Bw Kenyatta na Dkt Ruto akiwataja kama watu ambao hawafai kuongoza taifa kwa kuwa walikuwa wameshiriki umwagikaji wa damu 2007.

Aidha matamshi kama hayo ndiyo hasa yanaingiza jamii ya Mlima Kenya hofu kuhusu utawala wake, jamii hiyo ikishuku kwamba anaweza kugeuka na kulipiza kisasi kuhusu madhila ya miaka ya nyuma.

Rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta na makamu wa Rais wa kwanza marehemu Jaramogi Oginga Odinga walikuwa na uhasama mkubwa wa kisiasa miaka ya 60 na 70 na jamii hiyo imekuwa ikishuku kwamba Bw Odinga anaweza kulipiza kisasi.

Hofu hiyo ndiyo imekuwa ikifanya jamii hiyo kila mwaka wa uchaguzi kupiga kura kwa wingi kwa mpinzani mkuu wa Bw Odinga licha ya waziri huyo mkuu wa zamani kumpigia Mzee Mwai Kibaki kampeni kali na akawa Rais mnamo 2002.

Katika uchaguzi huo huo wa 2007, Bw Odinga kwenye kampeni zake alikuwa akisisitiza kuwa utawala wake utazingatia sana mfumo wa uongozi wa majimbo ambao ulikuwa unapendelewa sana na eneo la Pwani.

Hata hivyo, maeneo mengine hasa Mlima Kenya hayakuonekana kuridhia mfumo huo wa utawala ambao ulionekana ungewanyima nafasi ya kutawala kibiashara katika maeneo mengine ya nchi.

Kwa hivyo, Bw Odinga aendeleze kampeni yake kulingana na sera wala si matamshi yatakayowasaidia wapinzani wake wapate mwanya wa kumsawiri kama kiongozi hatari asiyefaa kupewa nafasi kuwa Rais wa Kenya.

You can share this post!

Wanachama 500 wagura UDA na kurejea ODM

MARY WANGARI: Utafiti mpya wahimiza manufaa ya kupokea...