CECIL ODONGO: Mbinu anazoweza kutumia Ruto ili kutwaa urais 2022

CECIL ODONGO: Mbinu anazoweza kutumia Ruto ili kutwaa urais 2022

Na CECIL ODONGO

NAIBU Rais Dkt William Ruto anafaa kujihusisha sana na kuvumisha umaarufu wake kupitia chama kipya cha UDA badala kuendelea kupigania udhibiti wa Jubilee ambayo imesalia kigae cha chama.

Wiki jana, Jubilee ilimpiga kumbo Dkt Ruto kwa mara nyingine kisiasa, baada ya kukatiza muafaka wa uchaguzi kati yake na PDP( sasa UDA) ulioafikiwa kuelekea 2017.

Hata hivyo, hatua hiyo ya Jubilee ilisitishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa baada ya UDA kuipinga na kupendekeza vyama hivyo viwili vipatanishwe kuhusu utata huo.

Kwa kuwa Dkt Ruto ashatangaza atatumia UDA kuwania Urais, ni vyema aanze mikakati ya kujiimarisha kisiasa badala ya kung’ang’ania ushirikiano na Jubilee ambayo imeonyesha wazi haimtaki kwa kumhujumu kila mara.

Kwanza, hata akiondoka Jubilee na asitangaze hivyo rasmi ila ajihusishe na siasa za UDA jinsi ambavyo amekuwa akifanya, hatavuliwa wadhifa wake wa Naibu Rais ambao ameshikilia tangu 2013Pili, Dkt Ruto ni mwanasiasa mkakamavu ambaye akiuza sera zake vyema, atakuwa pazuri kutwaa kiti cha Urais.

Kwa kuwa 2022 si mbali, kile ambacho Naibu Rais anafaa amakinikie ni kuhakikisha anadhibiti ngome yake ya kisiasa ya Bonde la Ufa, kisha asake uungwaji mkono katika maeneo yaliyopigia upinzani kura kupitia UDAAidha si siri kwamba ana uungwaji mkono eneo la Mlima Kenya ambalo lina kura nyingi zaidi nchini.

Iwapo atazungumza na viongozi wa eneo hilo na aridhie matakwa yao basi ataendelea kuwa kipenzi chao hadi 2022.? Kutokana na matukio ya kisiasa nchini, ni wazi eneo la Mlima Kenya halimshabikii Rais Kenyatta kutokana na serikali kufeli kutimiza miradi mingi iliyoahidi wakati wa kampeni za 2013 na 2017.

Eneo hilo sasa lipo nyuma ya Dkt Ruto.Mbinu nyingine ambazo Dkt Ruto anafaa akumbatie badala ya kushiriki mzozo na Jubilee, ni angalau kumnasa kiongozi moja wa One Kenya Alliance ( OKA) isipokuwa Gideon Moi ndipo apenye kisiasa maeneo yao.

Kwa kuwa ishara zote zinaonyesha kuwa mswada wa BBI utapita, anafaa kumtengea mmoja wao wadhifa wa Waziri Mkuu ambao utakwepo baada ya marekebisho ya katiba kupita.Akivutia kambini mwake Mabw Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula, angalau watamletea kura chache za Magharibi huku Kalonzo Musyoka akimzolea kura za Ukambani.

Viongozi hawa wa OKA ki uhakika wana nafasi finyu ya kushinda Urais wakilinganishwa na Dkt Ruto pamoja na Kinara wa ODM Raila Odinga. Itakuwa vigumu kwao kwa moja wao kukataa chambo cha Dkt Ruto ilhali wamekuwa nje ya serikali kwa zaidi ya miaka minane na wana ari ya kuingia serikalini.

Tayari kauli mbiu ya Wilbaro na mfuko mzito wa Dkt Ruto umemvunia uungwaji mkono na umaarufu miongoni mwa vijana na kumweka pazuri Kitaifa.

UDA pia kilitwaa kiti cha udiwani wa wadi ya London, Kaunti ya Nakuru mnamo Februari, ishara tosha kwamba imeanza kwenye mkondo wa kuridhisha.Bila Dkt Ruto, Jubilee haina umaarufu wowote na jinsi alivyoijenga ndivyo anafaa kuiasi na kupigania kupanua mawanda ya UDA kote nchini.

You can share this post!

Gavana hatarini kwa kumpa mkewe mamlaka ya kusimamia kaunti

Kesi ya ubakaji dhidi ya mbunge kusikizwa hadharani