CECIL ODONGO: Muungano wa Kalonzo hauna ushawishi kisiasa

CECIL ODONGO: Muungano wa Kalonzo hauna ushawishi kisiasa

Na CECIL ODONGO

MUUNGANO wa kisiasa unaopangwa kati ya baadhi ya viongozi wanaoongozwa na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi hautakuwa na ushawishi wowote hapa nchini kuelekea uchaguzi wa 2022.?

Kando na Mabw Musyoka na Mudavadi, muungano huo pia unajumuisha Gavana wa Kitui Charity Ngilu kupitia chama chake cha Narc na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula ambaye ni nyapara wa Ford Kenya.

Pia kuna fununu kwamba Seneta wa Baringo na kiongozi wa chama kongwe zaidi nchini Kanu Gideon Moi, yupo katika muungano huo.? Ukweli ni kwamba ushirikiano wa wanasiasa hawa japo ni mzuri kwa umoja wa nchi, si lolote si chochote kwa umaarufu wanaojivunia Naibu Rais Dkt William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga.

Kwanza, itakuwa vigumu kwa wanasiasa hao kumchagua moja wao kuwania Urais mnamo 2022 kwa kuwa kila moja wao ashatangaza kuwa atakuwa debeni na hawaonekani kuwa watalegeza msimamo.

Hata iwapo wameungana kwa kweli na ushirikiano wao udumu, ubashiri uliopo ni kwamba huenda wakamchagua Bw Musyoka au Bw Mudavadi kupeperusha bendera ya muungano huo.

Wengine kama Mabw Wetang’ula na Moi pamoja na Bi Ngilu hawana ufuasi wowote wa kushinda Urais kote nchini hata wakiungwa mkono na utawala uliopo.

Kulingana na utathmini ambao umekuwa ukitolewa na wadadisi wengi wa kisiasa Mabw Musyoka na Mudavadi hawana nafasi ya kushinda urais wakilinganishwa na Bw Odinga na Dkt Ruto.

Bw Musyoka hauziki nje ya ngome yake ya kisiasa ya Ukambani ambako pia umaarufu wake unatishiwa na magavana Dkt Alfred Mutua wa Machakos na Prof Kivutha Kibwana wa Makueni.

Bw Musyoka bado anasulubishwa na Wakenya hasa wafuasi wa ODM kutokana na kitendo chake cha kuungana na Rais Mstaafu Mwai Kibaki baada ya uchaguzi tata wa 2007 ambacho kilionekana kama usaliti mkubwa.

Wafuasi wa ODM bado wanaamini Bw Odinga alipokonywa ushindi kwenye kura hiyo na hatua ya Bw Musyoka kushirikiana na PNU na kuteuliwa Makamu wa Rais ulivuruga hesabu yao zaidi.? Bw Mudavadi naye hana umaarufu wa maana Magharibi mwa nchi japo tangu uchaguzi wa 2017, amekuwa akijikakamua kujijenga kama mwanauchumi wa kuokoa taifa hili kutoka kwa kiasi kikubwa cha deni linalodaiwa.

Kwa hivyo, Mabw Mudavadi na Musyoka wana kibarua kigumu kujijenga kisiasa ili umaarufu wao uhisiwe nje ya Magharibi na Ukambani mtawalia ambako wanadai ni ngome zao.

Aidha inadaiwa kwamba msingi wa kuungana kwao ni kumzuia Dkt Ruto kuingia Ikulu. Je, wataweza hili kivipi ilhali muungano wao hata haujatangaza mwaniaji wao wa kiti cha Urais?

Kwa sasa walio na nafasi ya kushinda urais ni Bw Odinga na Dkt Ruto kutokana na umaarufu si tu katika ngome zao za Nyanza na Bonde la Ufa, bali hata katika maeneo mengine nchini.

Ingawa siasa hubadilika na husemekana siku moja ni ndefu sana kwenye ulingo wa kisiasa, huu muungano wa Mabw Musyoka na Mudavadi bado hautoshi kuzidi umaarufu wa Dkt Ruto na Bw Odinga.

You can share this post!

Mamia Mlima Kenya waombea corona itokomee

Mbunge wa zamani wa Kaloleni afariki