CECIL ODONGO: Muungano wa Raila, Ruto utamtakasa Naibu wa Rais

CECIL ODONGO: Muungano wa Raila, Ruto utamtakasa Naibu wa Rais

Na CECIL ODONGO

HUKU madai yakiendelea kushika kasi kuhusu muungano unaonukia kati ya Naibu Rais Dkt William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga, kuna uwezekano mkubwa kwamba ushirikiano huo utamtakasa Dkt Ruto ambaye amekuwa akisawiriwa kuwa kiongozi fisadi.

Kuna kauli iliyozoeleka kutumiwa kuwa hakuna adui milele katika siasa ila iwapo Bw Odinga atakumbatia muungano huo hali hiyo itamsaidia Dkt Ruto kutokomeza dhana kuwa yeye ni mporaji na kiongozi mwenye tamaa ya mali ya umma.

Kati ya sakata ambazo Dkt Ruto amehusishwa nazo ni ile ya mahindi katika serikali ya muungano mnamo 2009, sakata ya ndege almaarufu Hustler Jet iliyogharimu Sh100 milioni, unyakuzi wa ardhi ya shule ya msingi ya Lang’ata kati ya nyingine.

Tangu uhasama wa kisiasa kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga uanze katika serikali ya muungano na baada ya uchaguzi wa 2013, wengi wa wafuasi wa upinzani wamekuwa na imani kwamba Dkt Ruto ni kiongozi fisadi asiyefaa kukaribia Urais wa nchi.

Japo Dkt Ruto hajawahi kushtakiwa kortini kwa kuhusishwa na baadhi ya sakata za ufisadi, ushirikiano wake na Bw Odinga iwapo utatimia utamfaa zaidi kisiasa.

Mara nyingi Bw Odinga amekuwa akiwatakasa viongozi ambao anashirikiana nao kutokana na ushawishi wake wa kisiasa na kuwafanya wafuasi wake wasahau madhila ambayo walitendewa hapo awali na wanasiasa hao.Baada ya uchaguzi wa 1997, taifa lilikuwa pabaya kiuchumi huku utawala wa aliyekuwa Rais marehemu Daniel Arap Moi ukikashifiwa kwa ufisadi na ukandamizaji wa haki.

Hata hivyo, Bw Odinga kupitia chama chake cha NDP alianzisha ushirikiano na Rais Moi na hata kujiunga na Kanu kisha akapokezwa wadhifa wa uwaziri.

Mtazamo wa Bw Odinga kuhusu uongozi wa Rais Moi ulibadilika ghafla na akawarai wafausi wake waunge mkono serikali.Licha ya kutakasa uongozi wa Rais Moi akitumai angepeperusha bendera ya Kanu katika uchaguzi wa 2002, Bw Odinga alimgeuka tena kiongozi huyo alipopendelea Uhuru Kenyatta wakati huo.

Bw Odinga pia alimtakasa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kuelekea uchaguzi wa 2013. Bw Musyoka alikuwa adui mkubwa wa wafuasi wa ODM hasa alipounga mkono upande wa PNU baada ya uchaguzi tata wa 2007. Hata walimpa lakabu ya tikitimaji kutokana na msimamo wake wa kukanganya kuhusu masuala mbalimbali.

Alifanya hivyo, baada ya kupokea uungwaji mkono wa Bw Musyoka 2013 na 2017 lakini sasa anaonekana amemtaliki kisiasa baada ya muungano wao wa NASA kuingia doa.

Katika awamu ya kwanza ya utawala wa Rais Kenyatta, Bw Odinga aliendeleza wimbi kali la upinzani dhidi ya serikali huku akifichua sakata mbalimbali zilizogubika serikali.

Hata hivyo, tangu aridhiane na Rais Uhuru Kenyatta kupitia handisheki mnamo Machi 31, 2018, Bw Odinga amefaulu kuwashawishi wafuasi wake kutupilia mbali msimamo wao mkali dhidi ya serikali.

Kwa hivyo, si siri kwamba ushirikiano wa Bw Odinga na Dkt Ruto utamnufaisha Naibu Rais na kutokomeza madai yaliyomsawiri kama kiongozi fisadi machoni pa wafuasi wa upinzani.

You can share this post!

Knec kuanza kusahihisha KCSE wiki hii

Gharama ya juu ya matibabu inavyobagua maskini