CECIL ODONGO: Ni kinaya Mudavadi kusaliti OKA ilhali hatakuwa debeni

CECIL ODONGO: Ni kinaya Mudavadi kusaliti OKA ilhali hatakuwa debeni

Na CECIL ODONGO

MNAMO Mei 20 1992, miezi saba pekee kabla ya uchaguzi mkuu, aliyekuwa mbunge wa Butere Martin Shikuku Oyondi alilazimika kujitetea hadharani baada ya kuandaa mkutano na Rais Daniel Arap Moi katika ikulu ya Nairobi.

Huu ulikuwa wakati ambapo siasa za uchaguzi mkuu wa 1992 zilikuwa zimenoga na wanasiasa wa mrengo wa Ford Kenya na Ford walikuwa wakiendesha kampeni kali za kumaliza utawala wa miaka 14 wa Rais Moi.

Bw Shikuku (sasa marehemu) wakati huo alikashifiwa kwa kuwasaliti wenzake na kuwa fuko wa serikali ndani ya upinzani.

Inadaiwa alikuwa akimtobolea Mzee Moi siri zote za mikakati ya kampeni ambazo vyama vya Ford Kenya chini ya Jaramogi Oginga Odinga na Ford Asili iliyokuwa ikiongozwa na Kenneth Matiba ilikuwa inaweka ili kumbandua rais huyo uongozini.

Mkondo huo wa usaliti umeshuhudiwa katika uliokuwa muungano wa OKA baada ya Kinara wa ANC Musalia Mudavadi kuwapiga wenzake chenga na kuingia katika ushirikiano na UDA.

Usaliti huo ulisababisha vinara wengine Gideon Moi (Kanu) na Kalonzo Musyoka wa Wiper, Cyrus Jirongo (UDP) kuwa wanasiasa pekee ambao wamesalia ndani ya OKA japo majuzi wamepigwa jeki na ujio wa Kinara wa Narc Kenya Martha Karua.

Mudavadi alimsaliti Bw Musyoka ambaye matokeo mbalimbali ya utafiti wa kamati iliyoteuliwa ndani ya OKA yalimweka kama mwaniaji bora wa muungano huo baada ya utathmini wa kina.

Itakumbukwa kuwa mnamo Januari 5, 2022 akiwa ameandamana na vinara wenzake, Bw Mudavadi alikanusha vikali madai kuwa ameingia katika muungano na Dkt Ruto.

Hata hivyo, tuhuma za usaliti zimekuwa zikizingira siasa za Bw Mudavadi tangu 2002 alipojiondoa kwenye mrengo wa LDP uliokuwa ukiwashirikisha waasi wa Kanu kisha kumuunga mkono Uhuru Kenyatta ambaye aliishia kupoteza uchaguzi huo kwa Mwai Kibaki.

Hii ilikuwa kinyume na mapenzi ya wengi wa wapigakura wa eneo anakotoka la Magharibi ambao walioongozwa na marehemu Kijana Wamalwa kumpigia Bw Kibaki kura.

Mnamo 2013, mbunge huyo wa zamani wa Sabatia aliamua kuelekea debeni licha ya wadadisi kusema kuwa ushirikiano wake na Bw Odinga ungemwezesha waziri huyo mkuu kuibwaga tiketi ya UhuRuto.

Kinaya ni kwamba Bw Mudavadi amesaliti wenzake ndani ya OKA ilhali kuna ishara kuwa hatawania Urais na atamuunga mkono Dkt Ruto.

Hata hivyo, siasa ni mikakati na licha ya usaliti unaozingira siasa zake, Bw Mudavadi ana haki ya kidemokrasia kuamua mkondo wa kisiasa anaouchukua bila kushurutishwa na yeyote.

  • Tags

You can share this post!

Mwingine afungwa miaka 24 jela kwa ufisadi

Rwanda kuandaa kikao cha marais wa Jumuiya ya Madola

T L