CECIL ODONGO: Ni unafiki viongozi wa Jubilee kumtoroka Raila

CECIL ODONGO: Ni unafiki viongozi wa Jubilee kumtoroka Raila

NA CECIL ODONGO

BAADHI ya wanasiasa kutoka Mlima Kenya walio katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya wameonekana kuanza mchakato wa kutemana kisiasa na kinara wa muungano huo Raila Odinga.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Jeremiah Kioni na aliyekuwa mbunge wa Nyeri, Bw Ngunjiri Wambugu wameonekana kutoa vijisababu ambavyo vinaweza kufasiriwa kama visivyo na mashiko huku wakidai kusalitiwa na ODM.

Kati ya masuala wanayodai ODM imewapigia kumbo ni uteuzi wa kamati mbalimbali za bunge, Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) na pia usimamizi wa muungano wenyewe.

Kutokana na kubadilika kwa misimamo ya wanasiasa nchini, inaafiki kusema kuwa nia ya wanasiasa hawa ni kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza ambao uko serikalini.

Kila baada ya uchaguzi wanasiasa wa upinzani hujiunga na upande uliopata ushindi wakidai kuwa hiyo ndiyo njia ya kuwapa watu wao miradi ya maendeleo.

Ukitathmini kwa undani, Jubilee inafaa iridhike na wema ambao wametendewa ndani ya Azimio.

Mwanzo katika EALA, vyama tanzu vikuu ndani ya Azimio vilipata nafasi kila kimoja.

Winnie Odinga atawakilisha ODM, Kennedy Musyoka (Wiper), Kanini Kega (Jubilee) na Suleiman Shahbal pia wa ODM.

Kwa hivyo, hapo hakuna kuonewa jinsi chama hicho cha Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kinavyodai.

Kwenye uongozi wa Bunge la Kitaifa, mbunge mteule Sabina Chege (Jubilee) alipokezwa wadhifa wa naibu kiranja wa wachache huku Fatuma Dullo (Isiolo, Jubilee) akiwa mwakilishi wa chama katika Tume ya Huduma za Bunge (PSC), cheo ambacho ni cha hadhi mno.

Isitoshe wabunge wa Jubilee walipokezwa nyadhifa katika kamati mbalimbali za bunge katika ugavi wa nafasi miongoni mwa vyama tanzu vya Azimio.

Kwa hivyo, ni unafiki mkubwa kwa Bw Kioni na Wambugu kudai kuwa Jubilee ilichezewa shere na ODM ilhali vyama vingine ndani ya muungano huo havilalamiki.

Pili, ukitathmini kura ambazo Jubilee iliahidi kuhakikisha Bw Odinga anajizolea Mlima Kenya, tofauti kati ya kura alizopata na idadi aliyoahidiwa ni kama usiku na mchana.

Hii ni licha ya kuwa hata mgombea mwenza-wake Martha Karua alikuwa akitoka eneo hilo la Mlima Kenya.

Ndiyo, Bw Odinga alipata kura 490,000 zaidi kuliko alizopata 2017, ila idadi hiyo haikufika milioni 2.4 ambazo aliahidiwa na Jubilee pamoja na wanasiasa Mlima Kenya wakati wa kampeni.

Katika uchaguzi huo, Jubilee yenyewe ilisombwa na mawimbi ya UDA katika ukanda wa Mlima Kenya na kwa jumla chama hicho kina wabunge 17 pekee.

Ni wazi kuwa nia ya wanasiasa wa Jubilee kama Bw Kioni na Ngunjiri ni kusaka mbinu ya kujiunga na upande wa serikali.

Hata hivyo, wanafahamu njia nzuri ya kufanya hivyo ni kuanza kumshambulia Raila na ODM ili wapokee makaribisho mazuri mrengo huo mwingine.

  • Tags

You can share this post!

Kenya yaagiza mbegu za GMO

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Morocco watoshana nguvu na...

T L