CECIL ODONGO: Ruto achunge ulimi wake, sifa ya ukabila inajitokeza

CECIL ODONGO: Ruto achunge ulimi wake, sifa ya ukabila inajitokeza

NA CECIL ODONGO

NAIBU wa Rais, Dkt William Ruto anafaa achunge ulimi wake kwenye kampeni anazoendeleza ili ajizuie kutoa kauli ambazo zinamsawiri kama kiongozi mkabila aliyejawa na uchu wa kulipiza kisasi.

Mnamo Jumamosi, Dkt Ruto alinukuliwa akiwaamrisha wakazi wa eneobunge la Kesses katika Kaunti ya Uasin Gishu, wasimchague tena mbunge wao Mishra Swarup kwa kumkaidi kisiasa. Aidha, Dkt Ruto alikashifiwa na wanasiasa wa muungano wa Azimio la Umoja kwa kumdunisha mgombeaji mwenza wao Martha Karua.

Kuhusu Bw Mishra, maneno aliyoyatumia Dkt Ruto ya kusema mbunge huyo alikuwa mwembamba alipochaguliwa 2017 na sasa hivi amekuwa kibonge hadi hawezi kutembea, hayafai kutoka kwa kiongozi wa hadhi ya Naibu Rais.

Ingawa ana haki ya kumpigia debe mwaniaji wa UDA katika eneobunge hilo, kauli aliyoitoa dhidi ya Bw Mishra inamsawiri Dkt Ruto kama kiongozi mkabila ambaye ana chuki kwa sababu mbunge huyo amekataa kufuata mwelekeo wake wa kisiasa.

Vilevile iwapo Dkt Ruto ana ushahidi kuwa mbunge huyo ni fisadi na amekuwa akila mali ya wananchi jinsi alivyosema, kwa nini hajachukua hatua kupiga ripoti katika asasi za uchunguzi kama tume ya EACC au kwa Idara ya Upelelezi (DCI)?

Ni kinaya kuwa Dkt Ruto anamkashifu Bw Swarup ilhali matokeo ya tafiti mbalimbali yamekuwa yakimuorodhesha kati ya wabunge wachapakazi ambao wanatumia vyema pesa za Hazina ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF).

Katika utafiti uliofanywa na kampuni ya Education Effect Africa mnamo Septemba 2020, Bw Mishra aliibuka wa tatu, nyuma ya Tim Wanyonyi (Westlands) na Otiende Amollo wa Rarieda katika utendakazi kwa raia.

Kati ya miradi ambayo amekuwa akiitekeleza ni kuipa kila familia isiyojiweza ng’ombe wa maziwa katika eneobunge lake.

Pia ameimarisha sekta ya afya kupitia hospitali zake za Mediheal na mara nyingi amewalipia wasiojiweza gharama ya matibabu.

Itakumbukwa kuwa anahudumu kama naibu mwenyekiti wa afya bungeni.

Kwa jumla, Bw Mishra amesawiriwa kama kiongozi mchapakazi kupitia miradi aliyokumbatia ya kuimarisha maisha ya wakazi na pia kuboresha miundomsingi katika eneobunge hilo.

Kwa hivyo, wakazi wa Kesses ndio walio na uamuzi wa kumchagua au kumtema kutokana na rekodi hiyo wala si eti kwa sababu amekosana na Dkt Ruto.

Ikizingatiwa kuwa Bw Mishra si Mkalenjin, Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) inafaa imwagize Dkt Ruto afike mbele yake kwa sababu kauli yake inafasiriwa kama ya kichochezi na huenda ikatatiza kampeni za mbunge huyo anayelenga kuhifadhi kiti chake.

Kukataa kumpa mbunge wa Nandi Hills, Alfred Keter tikiti ya UDA hata baada ya kushinda mchujo wa chama ni ithibati nyingine kuwa Dkt Ruto anathamini sana uadui na kisasi kuliko demokrasia.

Je atawavumilia wakosoaji wake ndani na nje ya serikali akifanikiwa kushinda urais?

Kwa sasa Dkt Ruto anafaa amakinikie kampeni zake na aichunge lugha anayotumia kuomba kura kwa sababu huenda ikamponza na kumpotezea ufuasi.

Ghasia zilizofuatia uchaguzi wa 2007 zinafaa ziwe funzo kwake. Vilevile asionekane kama aliyemtuma Seneta Mithika Linturi kutoa matamshi ya chuki Eldoret majuzi.

  • Tags

You can share this post!

NJENJE: Pakistan sasa yaongoza kwa ununuzi wa bidhaa za...

CHARLES WASONGA: IEBC, CA wakome malumbano ili kufanikisha...

T L