CECIL ODONGO: Ruto, Gachagua polepole wanaingia mtego wa Raila

CECIL ODONGO: Ruto, Gachagua polepole wanaingia mtego wa Raila

NA CECIL ODONGO

ITAKUWA vyema kwa utawala wa Kenya Kwanza (KK) kuzamia wajibu wao wa kuwatumikia Wakenya.

Rais William Ruto, naibu wake Rigathi Gachagua na viongozi wa KK wanapoteza muda na nguvu kumshambulia kinara wa upinzani, Bw Raila Odinga, badala ya kukabili changamoto zinazokabili wananchi.

Majukwaa ya maombi kila wikendi yamekuwa ya kumbeza Bw Odinga; hilo halifai kamwe.

Wikendi iliyopita, Rais na ujumbe wake wakiwa katika ibada kaunti za Trans Nzoia na Kirinyaga walitumia hotuba zao kumsuta kinara huyo wa muungano wa Azimio badala ya kueleza miradi watakayotekelezea wakazi.

Mwanzo, Rais na naibu wake wakumbuke watarejea kwa Wakenya baada ya miaka mitano kuomba kura.

Kitakachoamua kama watapewa nafasi ya kuongoza tena ni utendakazi wao, sio jinsi walimvamia Bw Odinga kwa maneno.

Kwa sasa, mtindo wa kumshambulia Waziri Mkuu huyo wa zamani hausaidii mwananchi wa kawaida aliyelemewa na ugumu wa maisha.

Wanachosahau ni kwamba Bw Odinga anatekeleza wajibu wake wa kuongoza upinzani kama ambavyo Rais na naibu wake wamekuwa wakitaka; kwa upande wao, kama serikali iliyo mamlakani wanapoteza muda na nguvu kutimiza jukumu lao pamoja na ahadi tele walizotoa za maendeleo.

Bw Odinga ni mwanasiasa shupavu anayejua siasa za maandamano zitashurutisha KK hadi wakubali kuridhiana naye.
Kisheria na kikatiba, kila raia ana haki ya kuandamana kwa amani anapohisi kudhulumiwa.

Ni jambo la wazi kama meno ya ngiri kuwa, tangu Kenya Kwanza watwae mamlaka maisha yazidi kuwa magumu mno licha yao kuahidi mambo yangeimarika.

Hata wafuasi wao wameanza kuchoshwa na utawala ambao umeanza kughairi ahadi uliowapa.

Je, Rais anatarajia upinzani unyamaze ilhali raia wanaendelea kuumia huku serikali ikionekana ni kama haijali kwa kufanya mambo ya kukuna kichwa, kama vile kuwaongezea ushuru?

Ndimi kali za viongozi wa Kenya Kwanza zisizoandamana na matendo zingepata pahali pa kutua wakati wa kampeni.

Uchaguzi uliisha na wapigakura sasa wanatarajia malipo kwa njia ya miradi ya maendeleo.

Alipoongoza kati ya 2002-2013, Rais Mwai Kibaki (sasa marehemu) alikuwa mchache wa maneno na mwingi wa vitendo; ndiposa alichapa kazi kuliko rais yeyote mwingine wa Kenya.

Ilikuwa nadra sana kumpata akijibizana na upinzani. MaBw Ruto na Gachagua watafanya vyema kuiga mfano huo wamakinikie maendeleo kwani Bw Odinga anatimiza upande wake.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali yafaa irahisishe harakati ya kuingia...

CHARLES WASONGA: Watahiniwa waliozoa gredi za chini wasife...

T L