CECIL ODONGO: Ruto na Raila wakome kushikilia misimamo mikali

CECIL ODONGO: Ruto na Raila wakome kushikilia misimamo mikali

NA CECIL ODONGO

RAIS William Ruto na kinara wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga wanastahili kuridhiana kwa ajili ya umoja wa nchi hasa baada ya uchaguzi mkuu uliopita.

Hii leo, Bw Odinga anatarajiwa kuandaa mkutano mkubwa wa kisiasa katika uwanja wa kihistoria wa Kamkunji, Nairobi anakotazamiwa kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa wafuasi wake baada ya kupoteza kura za Agosti 9, 2022.

Wikendi iliyopita, cheche kali zilishamiri kati ya viongozi hao hasa kuhusu Makamishina wanne waasi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) japo Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera na kamishina Justus Nyang’aya washajiuzulu kutoka kwa tume hiyo.

Mwanzo, Rais Ruto na Bw Odinga wanastahili kufahamu kuwa kila mmoja wao anajivunia ufuasi ambao ni sawa na nusu ya Wakenya na kauli zao huchukuliwa kwa uzito.

Rais Ruto hatawajibikia vyema nchi au kutimiza ajenda alizotoa wakati wa kampeni iwapo Bw Odinga atakuwa akiendeleza maasi dhidi yake mara kwa mara kupitia maandamano.

Utawala wa Kenya Kwanza unastahili kutambua kuwa Kenya ya sasa ni tofauti na ile ya miaka ya 60, 70, 80 au 90 wakati ambapo uongozi wa Kanu ulilaumiwa kwa udikteta na ukandamizaji wa haki za raia.

Tangu uingie mamlakani, utawala wa Kenya Kwanza umeonekana kuteka idara ya mahakama huku baadhi ya wanasiasa wa Kenya Kwanza waliokuwa na kesi kortini wakiondolewa mashtaka.

Pia kuna madai kuwa Rais Ruto anataka kudhibiti IEBC ili iwe rahisi kutetea wadhifa ifikapo 2027.

Ikiwa atakubali kufanya kazi na Bw Odinga, Rais Ruto hatakuwa wa kwanza kufanya hivyo mbali na kuwa hatua hiyo itasaidia kuleta utulivu nchini.

Marehemu marais Daniel arap Moi na Mwai Kibaki pamoja na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, wote walishirikiana na Raila na utawala wao ukawa haukumbwi na misukosuko au maandamano ya mara kwa mara.

Mnamo 1992, waziri huyo mkuu wa zamani alikuwa kati ya wanasiasa waliopigania mageuzi nchini na kuondoa utawala wa chama kimoja.

Kipindi hicho alikuwa hasimu wa kisiasa wa Mzee Moi.

Hata hivyo, baada ya uchaguzi wa 1997, aliridhiana naye na hata akajumuishwa serikalini.

Hali ilikuwa vivyo hivyo wakati wa utawala wa Kibaki hasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambao uliishia ghasia na mauaji ya zaidi ya Wakenya 1,000.

Raila na Kibaki waliunda serikali ya muungano iliyoongoza hadi 2013.

Pia baada ya kura za 2017 ambazo zilizingirwa na fujo na hata kiongozi huyo wa ODM kujiapisha kama Rais wa wananchi, Alishirikiana na Rais Kenyatta kupitia handisheki na Kenya ikawa na utulivu.

Kwa hivyo, si lazima Rais Ruto ampokeze Bw Odinga mamlaka katika utawala wake ila anaweza kushauriana naye mara kwa mara kuhusu masuala yanayoibua uhasama kati yao.

Raila ni mwanasiasa ambaye amejaaliwa uanaharakati na kutetea maslahi ya raia na utawala wa Kenya Kwanza ufahamu kuwa hautaendelea na ukandamizaji haki na kumtarajia kiongozi huyo wa upinzani kusalia kimya.

  • Tags

You can share this post!

Ushindi wangu wa Agosti 9 ulikuwa wa haki, asisitiza Lenku

ZARAA: Mwalimu anayejituma ili kufufua kilimo cha kahawa

T L