CECIL ODONGO: Sheria ikazwe kuadhibu wanaoeneza matokeo feki ya uchaguzi mitandaoni

CECIL ODONGO: Sheria ikazwe kuadhibu wanaoeneza matokeo feki ya uchaguzi mitandaoni

NA CECIL ODONGO

WAKENYA wanafaa kujifunza kutumia vyema mitandao ya kijamii kwa kuwa wengi huwa wanafuatilia habari ambazo huchapishwa huko kisha baadhi huzieneza bila kujali kama ni kweli.

Mara tu shughuli za kujumlisha kura kuanza mnamo Jumanne mchakato wa upigaji kura ulipotamatika, mabloga wa UDA walikesha mitandaoni usiku na kuchapisha habari kuwa baadhi ya wanasiasa hasa wa Muungano wa Azimio la Umoja walikuwa wameshindwa uchaguzini.

Hili lilikuwa linashangaza kwa sababu maeneo mengi ndio yalikuwa yameanza kuhesabu kura na hata katika kurasa za mitandao ya Tume Huru ya Uchaguzi Nchini (IEBC) bado kulikuwa hakuna chochote. Kwa mfano, baadhi ya wafuasi wa UDA walikuwa wametangaza kuwa mwaniaji wa ODM katika eneobunge la Lang’ata Fredrick Odiwuor maarufu kama Jalang’o alikuwa amebwagwa na mwenzake wa UDA.

Hata hivyo, ilipofika asubuhi, mwaniaji wa UDA Nixon Korir ambaye ndiye mbunge wa eneo hilo alikiri kuwa alikuwa amebwagwa na Bw Jalang’o.

Hali hiyo hiyo ilikuwa katika matokeo ya Urais ambapo watu walieneza propaganda kuhusu ushindani uliokuwepo kati ya Naibu Rais Dkt William Ruto na Kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga.

Wafuasi wa mirengo ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza pia walitumia mitandao vibaya kueneza matokeo ya uongo huku kila moja ikidai kuwa mrengo wake umeshinda.

Ili kuzuia matukio kama haya katika chaguzi zinazokuja, sheria inafaa kukazwa zaidi ili wale ambao wanaeneza propaganda zinazoweza kusababisha ghasia, wachukuliwe hatua kali ikiwemo kufikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka.

Pia muda ambao IEBC imepewa kutangaza matokeo ya Urais unafaa kupunguzwa kutoka siku saba hadi tano ili wajizatiti na kumaliza kazi yao kwa wakati kupunguza taharuki miongoni mwa wapigakura.

  • Tags

You can share this post!

Kiunjuri ahimili mawimbi ya UDA Mlima Kenya kushinda ubunge

TAHARIRI: Sheria yafaa ibadilishwe mshindi wa uchaguzi...

T L