CECIL ODONGO: Tumjuavyo huyu Kalonzo, atakunja mkia tu

CECIL ODONGO: Tumjuavyo huyu Kalonzo, atakunja mkia tu

Na CECIL ODONGO

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka anajipiga kifua bure kwa kudai kwamba, heri astaafu siasa kuliko kumuunga mkono Raila Odinga kwa mara nyingine katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Matamshi haya ya Bw Musyoka yangetolewa na mwanasiasa mwingine, kama Naibu Rais Dkt William Ruto, basi yangekuwa na mashiko kwa kiasi fulani kutokana na umaarufu anaojivunia kwenye siasa za kitaifa.

Ingawa ni uhuru wa makamu huyo wa raia wa zamani kuwania cheo chochote cha juu kisiasa, kudai kwamba liwe liwalo lazima awe debeni kwa kutumia jina la Bw Odinga, ni kujipendekeza kwa raia kisiasa. Mwanzo, Bw Musyoka amekuwa akijisawiri kama kiongozi asiyekuwa na msimamo dhabiti; akiwasubiri wanasiasa wengine wafanye maamuzi kuhusu masuala magumu kisha afuate mkondo.

Wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, Bw Musyoka – ambaye aliibuka katika nafasi ya tatu – alidai hadharani kwamba hangeungana na upande wa PNU, akitoa wito wa amani.

Siku chache baadaye, aliungana na mrengo wa Rais Mwai Kibaki na kuwaamuru wabunge wa chama chake wakati huo, ODM-Kenya, kuunga mkono serikali ya PNU.

Hadi leo wafuasi wa ODM hawajamsamehe, na wanaamini kwamba kuungana kwake na mrengo wa Bw Kibaki ndiko kulipunguza presha ya ODM kudai haki, baada ya kuhisi walipokonywa ushindi uchaguzini.

Kuelekea kura ya maamuzi ya 2010, Bw Musyoka alijizolea jina la tikitimaji baada ya kuchukua msimamo vuguvugu kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya ya sasa.Wakati huo akiwa waziri, mara alikuwa akisema anaipinga pamoja na mrengo wa ‘La’ wa Dkt Ruto; mara nyingine, akinukuliwa kuwa upande wa ‘Ndio’.

Haya matukio mawili ya 2007 na 2010 yanatosha kumsawiri Bw Musyoka kama kiongozi asiyekuwa na msimamo dhabiti kuhusu masuala muhimu Kitaifa. Hata yamechangia ubutu wake kisiasa hadi leo.

Ni kweli alimuunga mkono Bw Odinga 2013 na 2017, ila hilo halijamwongezea umaarufu wowote nje ya ngome yake ya Ukambani, ambako pia anakabiliwa na maasi makubwa.

Inashangaza kuwa kiongozi ambaye ana wabunge wasiozidi 20, anatangaza na kuapa hadharani kwamba hatamuunga mkono mpinzani wake; ambaye ana wabunge zaidi yake mara tatu, na ufuasi katika maeneo mengine kando na ngome yake ya Nyanza.

Aidha, Bw Musyoka kwa sasa hana gavana kwa tiketi ya Wiper eneo la Ukambani, baada ya Profesa Kivutha Kibwana kuvunja mkataba wa chama chake cha Muungano na Wiper.

Badala ya kujipiga kifua na hatimaye kulazimika kumeza maneno yake mwenyewe baadaye, Bw Musyoka anafaa kuweka mikakati ya kurejelea uongozi kwa kuwania angalau kiti cha ugavana, useneta au ubunge.

Japo wengi watafasiri hilo kama kujidunisha, angalau itamrejesha uongozini kwa mara ya kwanza tangu 2013; na kuzuia wanasiasa wengine wanaochipuka kwa nia ya kumaliza ushawishi wake Ukambani.

Ni jambo moja kutangaza kuwa unawania urais, na nyingine kushinda.Kutakuwa na faida gani Bw Musyoka awanie urais na aishie kushindwa kama 2007; au jinsi alivyobwagwa Musalia Mudavadi na ANC yake mnamo 2013?

Hata Muungano wao wa OKA pia hauna mashiko, na kumuuza kitaifa itakuwa kibarua.Heri hesabu zake zilenge kuunga mkono upande wa Dkt Ruto au Bw Odinga, kulingana na mrengo anaouona utashinda.

Hata Muungano wao wa OKA pia hauna mashiko na hata wenzake wakiamua awanie kiti cha Urais, kumuuza kitaifa kitakuwa kibarua kingine.

Siasa za sasa ni tofauti na alizozoea Bw Musyoka wakati wa utawala wa chama cha Kanu ambapo utiifu kwa Rais Daniel Arap Moi ndio ulimvunia kiongozi wadhifa wa kisiasa.

You can share this post!

AFYA: Je, virusi vya HIV vinachochea corona?

Jumwa atangaza kikosi chake 2022