CECIL ODONGO: Ushawishi wa mabaraza ya wazee kwenye mizani

CECIL ODONGO: Ushawishi wa mabaraza ya wazee kwenye mizani

Na CECIL ODONGO

MABARAZA ya wazee wa jamii yaliheshimiwa sana miaka ya zamani yalipotoa mielekeo ya kisiasa; lakini sasa hayana sifa hiyo tena.

Katika jamii mbalimbali mabaraza hayo yanashuhudia migawanyiko kwa sababu ya kutekwa na viongozi wa kisiasa.

Majuma mawili yaliyopita, Seneta wa Baringo Gideon Moi – ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha Kanu – alizuiwa na vijana kuingia eneo la Kapsisiywa, Nandi, kutawazwa na wazee waasi wa jamii ndogo ya Talai, kuwa msemaji wa jamii pana ya Kalenjin katika Bonde la Ufa.

Hii ilitokana na mzozo kati ya aliyekuwa mwenyekiti wa wazee hao Christopher Koyugi na mwenyekiti wa sasa, James Bassy. Wawili hao wametofautiana kuhusu nani kigogo wa Kalenji kati ya Bw Moi na Naibu Rais Dkt William Ruto.

Bw Moi amekuwa akivutana na Dkt Ruto kuhusu siasa za urithi za Bonde la Ufa na pia handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga.

Dkt Ruto alitawazwa na Mzee Bassy pamoja na wazee wa mrengo wake mwaka jana.Ni siri ya wazi kwamba wengi wa wazee wa kijamii wameweka kando jukumu la kutoa ushauri wa uongozi wa jamii, na kujali shibe yao huku wakipokea mihela ya wanasiasa ili kuendeleza ajenda zao.Ni hali inayoshuhudiwa sio tu kwa wazee wa Kalenjin.

Katika jamii ya Waluo, kulikuwa na tofauti kali kati ya mwenyekiti wa sasa, Bw Willis Otondi, na marehemu Riaga Omollo, uliochochewa na mustakabali wa siasa za eneo hilo ambazo zimetawaliwa na kigogo wa ODM, Bw Odinga, tangu kifo cha babake Jaramogi Oginga Odinga mnamo 1994.

Kabla ya mauti yake Agosti 2015, Mzee Omollo alikuwa akipinga siasa za Bw Odinga akidai zimechangia jamii ya Waluo kuwa kwenye upinzani kila baada ya miaka 10.Wakati huo ilidaiwa kwamba alikuwa akifadhiliwa na viongozi wa eneo hilo ambao walikuwa na ukuruba wa kisiasa na serikali ya Jubilee licha ya kuchaguliwa kwa tiketi ya ODM.

Tofauti baina ya Mzee Omollo na Bw Odinga zilianza 2010 baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kuongoza sherehe ya kutawazwa kwa Mzee Otondi katika uga wa Sony, Kaunti ya Migori.

Hali ni vivyo hivyo katika eneo jirani la Magharibi ambapo Baraza la Wazee wa Abaluhya wamekuwa wakitofautiana kuhusu umoja wa kisiasa wa jamii ya Mulembe.

Mara nyingi wazee hao wamevutana kuhusu nani anastahili kuwa msemaji wa kisiasa wa Mulembe, ikidaiwa kwamba mifuko yao imekuwa ikinenepeshwa kwa noti za wanasiasa wanaotoka nje ya jamii hiyo.

Katika eneo la Kaskazini Mashariki mambo ni tofauti kiasi kwani koo ndizo zina ushawishi, kiasi cha kuteua watakaowania nyadhifa za kisiasa kwa niaba ya mwananchi.

Kwa mfano, aliyekuwa seneta wa Mandera, Bw Billow Kerrow, na baadhi ya wabunge walikosa kutetea nyadhifa zao katika uchaguzi wa 2017 kama njia ya kutii maafikiano ya Baraza la Wazee wa Garre mnamo 2013.

Baraza hilo liliafikia uamuzi huo ili kuhakikisha koo ndogo pia zinapata nafasi ya kuongoza badala ya kubaguliwa na zile kubwa. Gavana Ali Roba naye alikaidi muafaka huo lakini bado alichaguliwa kuhudumu kipindi cha pili.

Yote tisa, mabaraza ya wazee yanafaa kutekeleza majukumu yao bila mapendeleo ili yadumishe hadhi yao, la sivyo ushawishi wao utayeyuka na mwishowe kupuuzwa na wananchi wakikumbatia viongozi wanaojali maslahi yao.

You can share this post!

MARY WANGARI: Elimu kuhusu afya ya uzazi itiliwe maanani...

Kero mitandaoni Balala akiteua Mwingereza kupigia debe...