CECIL ODONGO: Wakenya wadumishe amani wakisubiri matokeo ya kura

CECIL ODONGO: Wakenya wadumishe amani wakisubiri matokeo ya kura

NA CECIL ODONGO

WAKENYA wanaposubiri matokeo ya uchaguzi uliofanyika jana Jumanne, ni vyema wadumishe amani huku washindi kwenye nyadhifa mbalimbali wakiendelea kutangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC).

Kwa sasa, wengi wameelekeza macho yao kwa matokeo ya Urais huku wakiwa makini kumfahamu atakayechukua nafasi ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye anastaafu uongozini.

Hata hivyo, mchakato wa kupokea na kuhesabu kura ni jambo linalochukua muda na hakuna sababu ya kuwa na taharuki ila kuipa muda IEBC itekeleze wajibu wake.

Mwanzo, huu ni wakati ambapo wanasiasa wanastahili kuwatuliza wafuasi wao wasishiriki jambo lolote ambalo linaweza kusababisha utovu wa usalama au ghasia.

Iwapo kuna kiongozi ambaye hajaridhishwa na jinsi shughuli za kuhesabu kura zinavyoendelea, hafai kuwatumia wafuasi wake kuzua vurugu bali asubiri kufuata mkondo wa kisheria kuelekea mahakamani kutafuta haki.

Pili, Wakenya wajizuie kutumia mitandao ya kijamii kueneza propaganda au matokeo ambayo hayajathibitishwa au kutangazwa na IEBC.

Hii ni kwa sababu uvumi kama huo unaweza kusababisha taharuki na hata machafuko kwa wale ambao hawajaridhishwa.

Ni wakati huu ambapo vyombo vya usalama vinastahili kuwa ange na kuwachukulia Wakenya ambao wanaeneza propaganda hatua kali za kisheria kwa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka kortini.

Machafuko katika chaguzi za 2007 na 2017, yalitokea kwa sababu ya raia kukosa uvumilivu na viongozi kukosa kuhubiri amani.

Kwa hivyo, wanasiasa wenyewe, hasa wa UDA na Muungano wa Azimio la Umoja, wana jukumu kubwa la kuwatuliza wafuasi wao.

Ikizingatiwa kuwa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ilitoa orodha ya maeneo ambayo yapo kwenye hatari ya ghasia, ni vyema maafisa wa usalama katika maeneo hayo kuendesha shughuli zao kwa kufuata sheria.

Katika maeneo ya Kakamega na Mombasa ambapo wananchi hawakupiga kura za ugavana, ni vizuri kwa wawaniaji wa kiti hicho kuwatuliza raia, nayo IEBC iharakishe kutenga tarehe mpya ya uchaguzi katika kaunti hizo.

Viongozi wa ODM chama ambacho kinaonekana kuwa na ufuasi mkubwa katika kaunti hizo, hawafai kuwachochea raia kuzua ghasia.

Kule Kakamega, Fernandes Barasa wa ODM na Cleophas Malala wa ANC ambao walikuwa wawaniaji wakuu licha ya kughadhabishwa kwao, wanafaa kueneza amani.

Vivyo hivyo, Abdulswamad Nassir wa ODM na Hassan Omar wa UDA pia hawafai uhasama wao kugawanya raia kutokana na hilo suala la IEBC.

Kuaihirisha chaguzi katika maeneo hayo mawili kulionyesha kuwa IEBC haikuwa imefanya maandalizi ya kutosha.

Inasikitisha kuwa hii ni mara ya kwanza uchaguzi katika baadhi ya maeneo inaahirishwa huku Wakenya wakipiga kura kwa nyadhifa nyingine.

Wakenya nao wanafaa warejelee shughuli zao kama kawaida bila hofu zozote kwa sababu bado watahitaji kujikimu maishani.

Watu hawawezi wakalemewa kutimiza majukumu yao ya kusaka riziki eti wanasubiri matokeo ya uchaguzi mkuu.

Ingawa ina siku saba kumtangaza mshindi wa Urais, IEBC nayo isikawie kutangaza matokeo haya kama itakuwa imeyapata yote kwa kuwa hilo litasababisha wasiwasi mwingi na madai yaenezwe kuwa kuna udanganyifu ambao unaendelea.

  • Tags

You can share this post!

Jeremiah Kioni akubali kushindwa katika eneobunge la...

Man-United wajiondoa katika mbio za kumsajili fowadi Marko...

T L