CECIL ODONGO: Zipo dalili tele za mpasuko ndani ya One Kenya Alliance

CECIL ODONGO: Zipo dalili tele za mpasuko ndani ya One Kenya Alliance

Na CECIL ODONGO

MPASUKO unaonukia ndani ya One Kenya Alliance sasa unadhihirisha kuwa msukumo wa kubuniwa kwa muungano huo ulichochewa na maasi dhidi ya Kinara wa ODM Raila Odinga ndani ya NASA baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Haya sasa yamedhihirika kutokana na uhasama mkali wa kisiasa kati ya Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi ambao wote wametangaza wanalenga kuwania kiti cha Urais mnamo Agosti 9, 2022.

Vinara wengine wa muungano huo ni Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Cyrus Jirongo (UPF) na Gideon Moi (Kanu). Ingawa hivyo, hawa hawaonekani kumakinikia kuwania uongozi wa nchi.

Wiki jana, kamati iliyoteuliwa kuzamia utafiti kuhusu ni mwaniaji yupi maarufu kati ya vinara hao iliafikia kuwa Bw Musyoka ndiye mgombeaji bora zaidi kupeperusha bendera ya OKA.

Hatua hii inaonekana kumtia pabaya Bw Mudavadi ambaye akiwa katika Kaunti ya Nyamira wikendi iliyopita, alisisitiza kuwa atafika debeni liwalo na liwe.

Vivyo hivyo, mrengo wa Bw Musyoka umeonekana kushaajishwa na matokeo ya kamati ya OKA yaliyomweka nyapara wao mbele na haonekani kughairi nia huku akionekana kumakinikia Urais.

Kwanza, inashangaza kuwa OKA, muungano ulioonekana kama jukwaa la Mabw Mudavadi na Musyoka kung’aa kisiasa unaelekea kugeuka kigae kutokana na tamaa ya baadhi ya wanasiasa ndani yake.

Vinara wake walifanya kampeni pamoja na kuvishinda viti vya Useneta wa Machakos, ubunge wa Kabuchai na Matungu mapema mwaka jana.

Hata hivyo, ni ubinafsi kwa Bw Mudavadi kutomuunga mkono Bw Musyoka na kugeuka kuhusu nia ya awali ya OKA kuwa mwaniaji bora ataungwa mkono na wenzake.? Kukataa kwa makamu huyo wa Rais wa zamani kuunga mwenzake kunadhihirisha kuwa OKA ilikuwa tu ya kujiondoa kwenye NASA ambako Bw Odinga alikuwa na ushawishi mkubwa kuliko vinara wenzake.

Tiketi ya Kalonzo-Mudavadi japo haitakuwa na umaarufu sana wa kuwatikisa Naibu Rais Dkt William Ruto na Bw Odinga inaweza kuvutia kura za kuwanyima wanasiasa hao nafasi ya kupata asilimia 50 ya kura katika raundi ya kwanza.

Hata hivyo, iwapo Mbw Mudavadi na Musyoka kila moja atawania Urais kivyake basi wawili hao huenda wakasukumwa nje zaidi ikizingatiwa baadhi ya wanasiasa hasa wa ANC wamekuwa wakihama chama hicho na kujiunga na vuguvugu la Azimio la Umoja.

Kando na hayo itakuwa usaliti mkubwa kwa Mabw Musyoka na Mudavadi kukosa kushirikiana ndani ya OKA kisha mwishowe waishie kujiunga na mrengo wa Dkt Ruto au wa Bw Odinga.? Ingawa hivyo, hali ya kutoaminiana inayoendelea ndani ya OKA itadidimiza zaidi matumaini ya muungano huo kutoa mwaniaji wa urais.

Mabw Musyoka na Mudavadi wamewahi kuwania Urais 2007 na 2013 kivyao na walianguka vibaya katika chaguzi hizo mbili. ? Matukio hayo mawili yanafaa yawe funzo kwao ikizingatiwa wamekuwa nje ya serikali tangu 2013 na la muhimun ni wamakinikie kuingia serikali 2022 iwe kupitia mrengo wa Dkt Ruto au Bw Odinga au hata OKA yenyewe kama wanajiamini.

Kwa kuwa umri wao unasonga na wanasiasa chipukizi wanazuka katika ngome zao za kisiasa, vinara hao wawili wa OKA wakijikwaa kisiasa, basi huo huenda ukawa mwisho wao kisiasa.? Kutokana na jinsi mawimbi ya kisiasa yanavyoelekea OKA tayari wana nafasi finyu na umoja wao ungewasaidia kujiimarisha zaidi kisiasa kuliko mpasuko unaoendelea kuuzingira muungano huo kwa sasa.

  • Tags

You can share this post!

Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Miathene...

JUMA NAMLOLA: Wanaofanya Wakenya kuchukiana wasipewe nafasi...

T L