Michezo

Celta Vigo wadidimiza matumaini ya Barcelona kuhifadhi ubingwa wa La Liga msimu huu

June 27th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAO la dakika za mwisho kutoka kwa mvamizi matata mzawa wa Uhispania, Iago Aspas, 32, liliwawezesha Celta Vigo kusawazisha dhidi ya Barcelona na kuzamisha kabisa matumaini ya miamba hao wa La Liga kuhifadhi ubingwa wa msimu huu.

Ingawa Barcelona walipaa hadi kileleni mwa jedwali kwa alama 69, Real Madrid ambao wanajivunia alama 68 watafungua pengo la pointi mbili kileleni mnamo Jumapili ya Juni 28 iwapo watawatandika Espanyol uwanjani RCDE.

Kufikia sasa, Espanyol wanavuta mkia wa jedwali la La Liga kwa alama 24 na wapo katika hatari ya kushushwa ngazi kwa pamoja na Leganes na Mallorca wanaojivunia alama 25 na 26 mtawalia.

Luis Suarez aliwaweka Barcelona kifua mbele kunako dakika ya 20 kabla ya Fedor Smolov kusawazisha mambo kunako dakika ya 50 baada ya kukamilisha kwa ustadi krosi ya kiungo Okay Yokuslu. Bao lililofumwa wavuni na Suarez lilitokana na ushirikiano mkubwa kati yake na nahodha Lionel Messi.

Suarez alitikisa nyavu za Celta Vigo kwa mara ya pili kunako dakika ya 67 kabla ya aliyekuwa mchezaji mwenzake kambini mwa Liverpool, Aspas, kuyadidimiza matumaini ya Barcelona mwishoni mwa kipindi cha pili.

Celta Vigo ambao walikuwa wenyeji wa kivumbi hicho nusura wakizamishe kabisa chombo cha Barcelona kwa kufunga bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili ila kombora la Manuel Nolito, 33, mwishoni mwa kipindi cha pili likambabatiza kipa Andre ter Stegen wa Barcelona.

Messi ambaye kwa sasa hajafungia Barcelona bao lolote katika jumla ya mechi tatu ziliopita, anajivunia magoli 699 katika taaluma yake ya usogora kambini mwa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina. Goli la pili llilofumwa wavuni na Suarez lilikuwa la 250 kwa Messi kuchangia akivalia jezi za Barcelona.

Kufikia sasa, nahodha na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33 anaselelea kileleni mwa jedwali la wafungaji bora wa La Liga msimu huu kwa jumla ya mabao 21 na amechangia magoli mengine 17 muhula huu.