Celta Vigo yazamisha matumaini finyu ya Barcelona kutawazwa mabingwa wa La Liga muhula huu

Celta Vigo yazamisha matumaini finyu ya Barcelona kutawazwa mabingwa wa La Liga muhula huu

Na MASHIRIKA

KOCHA Ronald Koeman wa Barcelona anatarajia kwamba fowadi na nahodha Lionel Messi hajasakata mchuano wake wa mwisho uwanjani Camp Nou baada ya kikosi chake kupokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Celta Vigo mnamo Jumapili.

Matokeo hayo yalizamisha kabisa matumaini ya Barcelona ya kutawazwa wafalme wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu ikizingatiwa kwamba sasa ni pengo la alama saba ndilo linawatenganisha na Atletico Madrid wanaoselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 83.

Mkataba wa sasa kati ya Messi na Barcelona unatamatika rasmi mnamo Juni 30 na fowadi huyo raia wa Argentina bado hajaurefusha tangu afichue maazimio yake ya kuondoka ugani Camp Nou mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20.

Messi aliwaweka Barcelona kifua mbele dhidi ya Celta Vigo mnamo Jumapili kabla ya juhudi zake kuzimwa na magoli mawili kutoka kwa Santi Mina.

Kichapo hicho kina maana kwamba Barcelona kwa sasa watakamilisha kampeni za La Liga nje ya mduara wa mbili-bora kwa mara ya kwanza tangu 2007-08.

“Ni wazi kwamba ni vigumu kwa Barcelona kucheza dhidi ya kikosi chochote bila Messi kuwepo kikosini. Ndiye mchezaji bora zaidi duniani. Tayari amefunga mabao 30 na kuvunia kikosi idadi kubwa ya alama msimu huu,” akatanguliza Koeman.

“Messi pekee ndiye mwenye jibu la swali la iwapo atasalia au kuondoka ugani Camp Nou. Ni matarajio ya kila mmoja wetu kikosini kwamba atatia saini mkataba mpya,” akasema kocha huyo raia wa Uholanzi.

Koeman alikataa kujibu maswali kuhusu mustakabali wake mwishoni mwa mechi dhidi ya Celta Vigo huku magazeti mengi nchini Uhispania yakidai kwamba mwanasoka wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez alikuwa amezungumziwa na usimamizi mnamo Mei 15, 2021 kuhusu uwezekano wa kukubali mikoba ya ukocha ugani Camp Nou kuanzia msimu ujao.

“Anayejua jibu la swali kuhusu mustakabali wangu kambini mwa Barcelona ni mwajiri wangu. Nitaheshimu maamuzi yoyote,” akasema kocha huyo wa zamani wa Everton na Southampton.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

UDAKU: Dele Alli si mchache! Ameingiza boksi binti wa kocha...

Jubilee yapiga kampeni kali za kupangua UDA uchaguzini Rurii