Chager aashiria kushindwa

Chager aashiria kushindwa

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA mtetezi wa Mbio za Magari za Kitaifa nchini Kenya (KNRC) Baldev “Boldy” Chager anaonekana kusalimu amri mapema baada ya kukiri itakuwa vigumu kuzima kiongozi Carl ‘Flash’ Tundo kutwaa taji msimu huu katika duru ya mwisho ya KCB Guru Nanak Rally.

Chager ana nafasi ndogo ya kutetea ubingwa aliopata 2019 kabla ya msimu 2020 ukatizwe kwa ghafla ya mkurupuko wa virusi vya corona.Chager, ambaye pia anafahamika kwa jina la utani kama “Flying Singh”, anahitaji ushindi pekee wa Guru Nanak na kuomba kuwa Tundo atateleza katika duru hiyo itakayofanyika katika eneo la Ilbisil katika kaunti ya Kajiado na kuandaliwa na klabu ya Sikh Union Nairobi.

Duru hiyo imehamishwa kutoka eneo la Stoni Athi katika mji wa Athi River, kaunti ya Machakos kutokana na hali mbaya ya anga.Afisa anayehusika na barabara za duru hiyo Onkar Kalsi aliongeza kuwa barabara kamili za mashindano zitatangazwa wakati wowote kutoka sasa.

Tundo, ambaye anatetea taji la Guru Nanak Rally aliloshinda Februari 2020, anahitaji kumaliza duru hiyo katika nafasi ya nane pekee kunyakua ubingwa wa kitaifa kwa sababu yuko alama 25 mbele ya mpinzani wake wa karibu Chager.

Bingwa huyo mpya wa Afrika atazoa alama 11 kutoka Guru Nanak akimaliza katika nafasi ya nane na 177 kwa jumla. Alama zote za Chager anaweza kutia kapuni msimu huu akitawala Guru Nanak kwa alama za bonasi ni 176.Hata hivyo, Tundo akimaliza nje ya mduara wa nane-bora ama akose kukamilisha duru hiyo, basi Boldy ataibuka mshindi muradi pia yeye amalize Guru Nanak katika nafasi ya kwanza.

“Lazima tuzime Tundo kwa alama 25 ambayo ni kitu kigumu sana. Hata akitumia gia ya tatu, atapata pointi anazohitaji kushinda msimu huu. Pengine kitu kibaya kimtendekee hapo ndipo tutapata mwanya, lakini kwa sasa tuna nafasi finyu sana.

Hata hivyo, tutapaisha gari kisawasawa jinsi tunavyofanya kila mara na kutafuta mafanikio kwenye Guru Nanak…,” alisema Chager.Chager atashirikiana na Ravi Chana katika gari la Volkswagen Polo R5 naye Tundo atatumia Mitsubishi Lancer Evolution 10 na kuelekezwa na Tim Jessop.

Mwanadada Maxine Wahome katika msimu wake wa kwanza wa KNRC katika daraja ya pili, yumo mbioni kutwaa taji la kitengo hicho. Anaongoza kwa alama 137 akifuatiwa na Daren Miranda (123), Hamza Anwar (84) na Evans Kavisi (73).

You can share this post!

Caf: Maswali tele kuhusu maandalizi ya Tusker, Gor

Kaunti yatishia kushtaki Wizara ya Utalii kwa Rais

T L