Chaguzi ndogo kuamua vigogo wa siasa Magharibi

Chaguzi ndogo kuamua vigogo wa siasa Magharibi

Na CECIL ODONGO

HATIMAYE raia wa maeneobunge ya Matungu na Kabuchai wataingia debeni Machi 4 kuwachagua wabunge wapya huku muda wa kampeni nao ukikamilika rasmi leo.

Wawaniaji wamejivumisha kwa wananchi na sasa raia ndio wana jukumu la kuamua watakaowahudumia kwa muda uliosalia katika Bunge la Kitaifa kabla ya kura ya 2022.

Siasa za eneobunge hilo hata hivyo, zinatarajiwa kuonyesha nani mbabe wa siasa za Magharibi kati ya Kinara wa ANC Musalia Mudavadi, Moses Wetang’ula wa Ford Kenya na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya.

Bw Mudavadi amekuwa akimvumisha sana mwaniaji wa chama chake Peter Nabulindo huku akikusudia kusalia na kiti hicho kilichokuwa kikishikiliwa na marehemu Justus Murunga pia wa chama hicho.

Kwa upande mwingine, kiti cha Kabuchai kilikuwa kikishikiliwa na marehemu James Mukwe kupitia chama cha Ford Kenya. Bw Wetang’ula amekuwa akimvumisha Majimbo Kalasinga japo amekuwa akipokea upinzani mkali kutoka kwa mwaniaji wa UDA Evans Kakai.

Katika eneo la Matungu, ubabe hasa upo kati ya Bw Mudavadi na Gavana Oparanya ambaye amekuwa akimuunga mkono mbunge wa zamani David Were.

Ushindi kwa ODM utadhihirisha kwamba naibu huyo wa zamani wa waziri mkuu bado ana kibarua kigumu kuhakikisha umoja wa jamii wa Waluhya.

Pia ushindi huo utakweza hadhi ya siasa za Bw Oparanya ambaye amekuwa akisifiwa kutokana na rekodi ya kuridhisha ya maendeleo tangu achaguliwe gavana 2013.

Tayari Bw Oparanya ametangaza kwamba analenga kuwania Urais na kwa kuwa amekuwa mstari wa mbele kumvumisha Bw Were eneo la Matungu, ushindi huo utamsawiri na kumwongezea alama anapozamia siasa za kitaifa.

Kwa upande mwingine ubabe wa Mabw Mudavadi na Oparanya katika siasa za eneo hilo utavurugwa zaidi iwapo Bw Alex Lanya anayewania kupitia UDA ya Naibu Rais Dkt William Ruto atapata ushindi.H

ali ni vivyo hivyo kwa Bw Wetang’ula ambaye anadaiwa kuwa na usemi mkubwa katika siasa za Bungoma hasa kaunti za Trans Nzoia na Bungoma. Ford Kenya ilikuwa na wabunge watatu katika Kaunti ya Bungoma baada ya uchaguzi wa 2017.

Hata hivyo, ni marehemu Bw Mukwe pekee aliyekuwa mwaminifu kwa chama baada ya Wafula Wamunyinyi wa Kanduyi na Dkt Eseli Simiyu wa Tongaren kutekeleza mapinduzi dhidi ya Bw Wetang’ula.

Itakuwa hatari iwapo waziri huyo wa zamani atapoteza kiti cha eneobunge la nyumbani kwa mwaniaji anayevumishwa na Naibu Rais ambaye amekuwa akitembelea eneo hilo kila mara kuwashawishi raia wamuunge mkono 2022.

Kwa hivyo siasa za Mabw Mudavadi, Wetang’ula na Oparanya zitaathirika kwa njia mmoja au nyingine iwapo watapoteza viti hivyo kwenye uchaguzi huo mdogo wa Alhamisi.

Kampeni zimekuwa na amani na sasa ni wakati wa raia pia waamue kwa njia ya amani bila vurugu au ghasia kushuhudiwa wakati wa upigaji kura na kutolewa kwa matokeo.Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nayo inafaa iwe macho ili kuzuia visa vyovyote vya udanganyifu ambavyo vitachangia kuvurugwa kwa sauti ya raia debeni.

You can share this post!

Serikali yaahidi kulinda chanjo ya corona dhidi ya matapeli

Raila atua Pwani kufunza wakazi kusakata Reggae