Michezo

Chai ya mwisho aliyoitiwa Pochettino kabla ya kufungishwa virago

May 22nd, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

KOCHA Mauricio Pochettino alikunywa chai na bwanyenye wa Chelsea, Todd Boely siku chache kabla ya kuamua kuagana na klabu hiyo baada ya kuwa usukani kwa miezi 11.

Raia huyo wa Argentina ameondoka kwa hiari baada ya kuifikisha timu hiyo katika fainali ya Carabao na nusu-fainali ya FA Cup, lakini anadai kuna watu fulani wenye uwezo mkubwa katika klabu hiyo walitaka aondoke.

“Ni kawaida hapa makocha kuondoka kila wakati kwa sababu wenyewe wanataka mataji,” alisema kocha huyo.

Wiki chache zilizopita, kocha huyo aliiwezesha klabu hiyo kushinda mechi sita mfululizo na kumaliza katika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyomalizika Jumapili iliyopita.

Taarifa rasmi kutoka kwa klabu hiyo ilisema: “Chelsea FC imekubali kuagana na Pochettino kwa hiari.”

Pochettino alisema: “Asanteni sana wamiliki wa Chelsea na wakurugenzi wa michezo klabuni kwa kunipa nafasi kufanya kazi katika klabu hii yenye historia kubwa. Bila shaka nimeondoka wakati klabu iko katika hali nzuri ya kuvuma zaidi msimu ujao, na barani Ulaya kwa jumla,” alisema kocha huyo aliyeondoka pamoja na wasaidizi wake, Jesus Perez, Miguel d’Agostino, Toni Jimenez na Sebastiano Pochettino.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 52 alikuwa ameinoa Chelsea kwa miezi 11, baada ya kuteuliwa mwezi Mei akijaza nafasi iliyoachwa na jagina Frank Lampard baada ya klabu hiyo kufanya usajili wa nguvu.

Kabla ya kumuajiri, Chelsea ilitumia zaidi ya Sh67 bilioni kununua wachezaji wapya, wengi wao wakiwa chini ya umri wa miaka 25.

Klabu hiyo pia iliwauza wachezaji kadhaa wakiwemo Cesar Azpilicueta, N’Golo Kante na Mateo Kovacic na kupata Sh42 bilioni.

Baada ya kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Bournemouth, Jumapili, Pochettino alitangaza mpango wa kuondoka na kutafuta maisha mapya kwingine.

Wakurugenzi wa Michezo katika klabu hiyo, Laurence Stewart na Paul Winstanley walisema: “Kwa niaba ya Chelsea, tungependa kumpongeza Mauricio kutokana na juhudi zake alipokuwa kocha mkuu wa klabu hii kwa msimu mmoja.”

“Tutamkaribisha tena ugani Stamford Bridge wakati wowote atakapotaka kurejea na tunamtakia kila la heri maishani.”

Awali, Pochettino alisaidia klabu ya Paris Saint-Germain kutwaa ubingwa wa Ligue 1 alipokuwa nayo kwa miezi 18, baada ya kumaliza zaidi ya miaka mitano akiwa na Tottenham Hotspur, na kuifikisha katika fainali ya Klabu Bingwa barani Ulaya mnamo 2019.

Kocha Kieran McKenna wa Ipswich, Enzo Maresca wa Leicester City, Sebastian Hoeness wa Stuttgart, Miguel Angel Sanchez Munoz wa Girona na Thoams Frank wa Brentford ni miongoni mwa makocha wanaofikiriwa kujaza nafasi hiyo.

Pochettino anatarajiwa kuongoza kikosi cha World XI katika mechi ya maonyesho itakayochezewa Stamford Bridge mapema mwezi ujao.

Huenda akajiunga na Manchester United ambao wamekuwa wakimtafuta kwa muda mrefu.