CHAKICACA: Chama imara kuhusu makuzi ya Kiswahili shuleni Carmelvale Catholic

CHAKICACA: Chama imara kuhusu makuzi ya Kiswahili shuleni Carmelvale Catholic

Na CHRIS ADUNGO

TANGU kuasisiwa kwa Chama cha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Carmelvale Catholic (CHAKICACA), Nairobi mnamo 2015, chama kimepata mashiko na mwamko mpya kiasi cha kuwafanya wanafunzi wengi kukichapukia Kiswahili.

Kwa hakika, chama hiki kimepania kuwa bakora bora dhidi ya matokeo mabaya katika mtihani huku kikiazimia pia kukomesha mtazamo hasi kuwa Kiswahili ni somo gumu miongoni mwa wanafunzi katika gatuzi la Nairobi.

Mwalimu Engido na mwenzake Bw Zadock Amakoye wana wingi wa matumaini kwamba wanachama wa CHAKICACA ambao wanatarajia kuufanya mtihani ujao wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) watafaulu vyema katika somo la Kiswahili.

Walimu hawa wamekuwa mihimili katika kuimarisha chama kwa kuwatia shime wanafunzi na kuwakuza katika fani mbalimbali za uandishi wa kazi bunilizi.

“Chama kimekuwa mlezi wa matokeo bora ya Kiswahili miongoni mwa wanachama. CHAKICACA kwa sasa kimesajili zaidi ya wanachama 300 ambao hujitolea kwa hali na mali kushiriki shughuli zote za chama kikamilifu,” anasema Bw Amakoye.

Wakati wa kalenda ya kawaida ya masomo shuleni, wanachama hukutana kila siku ya Jumatano kuanzia saa kumi jioni katika mojawapo ya madarasa kwa lengo la kujadili shughuli za maendeleo ya chama.

Wakutanapo, wanachama hufaidi pakubwa kutokana na mijadala mipevu ya Kiswahili inayohusu masuala ibuka na teknolojia. Mbali na kuwasilisha mashairi na kubuni mikakati kabambe ya kuimarisha chama, wao pia hujadili maswali tatanishi waliyokumbana nayo madarasani katika kipindi cha wiki nzima ya awali.

Wanachama waliojibu swali la wiki kwa usahihi hutuzwa.Kilipobuniwa, CHAKICACA kilikuwa na lengo moja kuu la kuboresha matokeo ya somo la Kiswahili yaliyokuwa yakiendelea kudorora shuleni Carmelvale Catholic.

Mbali na hilo, chama kiliazimia haja ya kuendeleza tamaduni za Kiswahili shuleni, kusaidia wanachama katika marudio na utafiti pamoja na kulea vipaji vya utunzi wa kazi za kibunifu miongoni mwa wanafunzi.Chama hiki kimekuwa kikiandaa makongamano mengi ya kwa minajili ya kuchangia makuzi ya Kiswahili katika majukwaa tofauti.

Zaidi ya kuandaa makongamano ya ndani kwa ndani, wanachama wanajivunia pia kuhudhuria warsha mbalimbali ndani na nje ya Kaunti ya Nairobi.Jivunio la CHAKICACA kwa muda mfupi wa uwepo wake ni kuwakuza washairi na wanahabari wengi chipukizi.

Masomo ya kawaida kwa wanafunzi wote yatakaporejea shuleni kuanzia Januari 2021, Bw Amakoye anakariri kuwa watapania kuanza kuigiza michezo mbalimbali chini ya uelekezi wa walimu katika Idara ya Kiswahili shuleni Carmelvale Catholic.

Wanachama pia wataazimia kutunga mashairi kwa minajili ya kuchapishwa katika gazeti hili la Taifa Leo na kutunga nyimbo za kuhamasisha jamii kuhusu njia mbalimbali za kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa korona.Kwa upande mwingine, wanachama wanakumbuna na matatizo si haba.

Tatizo kubwa zaidi wanalokumbana nalo ni ukosefu wa vitabu vya kutosha maktabani.Mahali pa mkutano ni donda ndugu ikizingatiwa kwamba wanakutana madarasani ambapo wanafunzi wenza ambao hushiriki michezo nyakati za jioni, huwasumbua wanapoendelea na vikao vyao.

Licha ya changamoto hizo, wanachama wamejitolea kuhamasishana kuhusu umuhimu wa kuwa mabalozi wa lugha hii ashirafu ya Kiswahili. Nia yao ni kufanya Carmelvale Catholic kuwa kisiwa cha Kiswahili sanifu katika uzungumzaji na uandishi wa kazi za kibunifu.

You can share this post!

Kayole Starlets yajipanga kutifua vumbi la kufa mtu

KINA CHA FIKIRA: Shirikiana na watu bora ili nawe uwe bora,...