Makala

CHAKILOKI: Chama ngangari katika makuzi ya Kiswahili Shule ya Upili ya Loreto Kiambu

March 6th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

CHINI ya ulezi wa Bi Jacinta Nyambura Thuku, Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Loreto Kiambu (CHAKILOKI) kiliasisiwa mwanzoni mnamo mwaka 2010 kwa nia ya kuangazia kwa kina stadi za Kusikiliza, Kuzungumza, Kusoma na Kuandika.

Madhumuni mengine yaliyochochea kuasisiwa kwa CHAKILOKI ni haja kubwa ya kukwamua shule ya Loreto Kiambu kutokana na msururu wa matokeo mabaya katika somo la Kiswahili, kubadilisha mtazamo hasi wa wanafunzi kuhusu Kiswahili, kukuza talanta za wanafunzi katika kazi za kubuni, kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kushirikiana na vyama vingine ili kuboresha na kuimarisha matokeo ya Kiswahili ya KCSE.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Loreto, Kiambu (CHAKILOKI). Picha/ Chris Adungo

Chama kina mikakati ya kushiriki makongamano mbalimbali ya Kiswahili kwa maazimio ya kuwakutanisha wanafunzi na walimu maarufu wa Kiswahili, wanahabari na waandishi mashuhuri ambao kwa wengi ni vielelezo.

Baadhi ya wanafunzi waligundua kwamba wana udhaifu wa kujieleza kwa ufasaha kimazungumzo kwa kutumia lugha sanifu ya Kiswahili.

Mbali na hayo, chama hiki vilevile kinawapa wanafunzi fursa ya kuendesha midahalo wazi ili kuangazia masuala mbalimbali yanayofungamana na maendeleo ya jamii kwa jumla pamoja na changamoto zinazowakabili wanafunzi masomoni.

Warsha za aina hii huandaliwa ndani na nje ya shule huku uzingativu zaidi ukielekezwa katika kujadili masuala kama vile haki za watoto, matatizo yanayowakumba vijana, uongozi katika jamii na nafasi ya vijana katika kuendeleza taifa na utamaduni wa Kiswahili.

CHAKILOKI kinanuia kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaweza kuzungumza lugha sanifu ya Kiswahili bila ya kuathiriwa na tafsiri za moja kwa moja katika mengi ya maneno.

Wanachama wanafanya juhudi za kutumia misamiati mwafaka ya Kiswahili katika kuelezea dhana zenye utata miongoni mwa watumiaji wa lugha hiyo.

Uzungumzaji na Usikilizaji ni stadi ambazo wanafunzi hawa huzihitaji sana ili kuendesha mijadala yenye mantiki.

Vikao

Chama hundaa vikao mara kwa mara kwa lengo la kutoa jukwaa bora kwa wanafunzi kuhamasishana, kukumbushana mambo ambayo yalifundishwa darasani na kuzamia kwa kina baadhi ya mada ambazo zinawatatiza madarasani, hasa katika somo la Kiswahili.

Aidha, wanachama huazimia haja ya kudhihirisha upekee wa vipaji vyao katika kutunga na kughani mashairi, kutegua vitendawili na hata kutamba hadithi.

Vinara wa CHAKILOKI wana mipango ya kuhakikisha kuwa wanapata uanachama wa kila mwanafunzi shuleni hasa ikizingatiwa kwamba Kiswahili ni somo la lazima na la kutahiniwa katika kiwango cha KCSE.

Kupitia CHAKILOKI, wanafunzi wa Loreto Kiambu kwa sasa wananuia kuingia katika Shindano la Uandishi wa Insha linaloendeshwa na gazeti hili la Taifa Leo.