CHAKISTA mwenge thabiti wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya State House Girls

CHAKISTA mwenge thabiti wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya State House Girls

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya State House Girls, Nairobi (CHAKISTA) kipo mstari wa mbele kuhakikisha kwamba matumizi ya Kiswahili Sanifu yananavumishwa huku makuzi ya lugha yenyewe yakipigiwa chapuo na wanafunzi kwa ushirikiano na walimu wao.

Kwa sasa, chama hiki kipo chini ya ulezi wa Bw Kevin Chisaka na mwalimu Solomon Maraga. Wanachama huandaa vikao kila Jumatano ili kujadili mikakati ya kuendeleza chama na kuzamia baadhi ya mada za zinazowatatiza katika somo la Kiswahili.

Chama kiliasisiwa kwa madhumuni ya kukuza lugha ashirafu ya Kiswahili na kutoa jukwaa mwafaka la kuwaondolewa wanafunzi dhana potovu kwamba Kiswahili ni somo gumu.Ni matumaini ya Bw Chisaka na Bw Maraga kwamba kuwepo kwa CHAKISTA kutabadilisha mtazamo hasi miongoni mwa wanafunzi kuhusu Kiswahili.

Malengo mengine ya chama hiki ni kukuza vipaji mbalimbali vya wanafunzi katika sanaa za uigizaji, utangazaji, ulumbi, uandishi wa hadithi na utunzi wa mashairi. Ili kuwapa wanafunzi nafasi maridhawa ya kukichangamkia Kiswahili ipasavyo, shughuli zote katika Shule ya Upili ya State House Girls huendeshwa kwa Kiswahili kila Ijumaa.

Wanachama huwatangazia walimu na wanafunzi wenzao habari na matukio mbalimbali gwarideni huku masuala ibuka yakipewa kipaumbele.Chama kimepania pia kuwahimiza wanafunzi kuendelea kushiriki makongamano mbalimbali ya Kiswahili huku wanachama wakisisitiziwa haja ya kushiriki mashindano mbalimbali ya Kiswahili hasa Uandishi wa Insha katika gazeti hili la Taifa Leo.

CHAKISTA kimeanza kuzaa matunda ikizingatiwa kwamba kimeamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanachama ambao kwa sasa ni mabalozi halisi wa lugha hii na wasomaji wakubwa wa Taifa Leo.

Chama pia kinalenga kuanzisha harakati za kuchapisha Jarida la Kiswahili kwa lengo la kuzua mijadala muhimu kuhusu Kiswahili na kuwapa wanafunzi jukwaa la kujieleza na kutononoa vipaji vyao katika sanaa ya uandishi wa kazi bunilizi.

Usimamizi wa CHAKISTA unatambua juhudi za Mwalimu Mkuu Bi Evelyne Nabukwesi pamoja na walimu wote wa Kiswahili chini ya uelekezi wa Bi Florence Mboya ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya State House Girls.

You can share this post!

Kenya yakusudia kuchanja raia 5m kufikia Desemba

Mali ya Sirma hatarini kuuzwa na madalali

T L