Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Miathene (CHAKIMIA)

Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Miathene (CHAKIMIA)

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Miathene (CHAKIMIA) sasa kinajivunia zaidi ya wanachama 150.

Chama hiki ni jukwaa mwafaka kwa wanafunzi kupiga jeki shughuli za Idara ya Kiswahili katika juhudi za kuboresha matokeo ya KCSE na kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili shuleni.

Waasisi wa CHAKIMA ni Bw Japhet Karundu na Bw Kenneth Mwenda – walimu wanaoshirikiana na wenzao Bw William Mwirigi, Bw Nelson Mandela, Bi Purity Kathure, Bi Diana Kendi na Bw Kimathi Mworia kusukuma gurudumu la Kiswahili katika shule hii iliyoko Tigania Magharibi, Kaunti ya Meru.

Mwalimu Mkuu, Bw Njue Rose, naye yuko mstari wa mbele kufaulisha maazimio ya chama kwa kuhakikisha kuna vitabu vya kutosha vya Kiswahili katika maktaba.

Zaidi ya kuboresha matokeo ya Kiswahili katika KCSE, chama pia kinakuza talanta za wanafunzi katika sanaa za uigizaji, utunzi wa mashairi na uandishi wa kazi bunilizi.

Chama kimechangia pakubwa kuwavusha wanafunzi katika masuala ya kiakademia. Vikao vya mara kwa mara vinavyoandaliwa na wanachama huwapa fursa za kuzamia baadhi ya mada zinazowatatiza katika somo la Kiswahili chini ya uelekezi wa walezi na vinara wao.

Chama kinaazimia kuandaa wanafunzi watakaokubalika kitaifa na kimataifa kutokana na weledi wao katika masomo ya lugha. Baadhi ya shughuli za wanachama ni kukusanya habari na kuzisoma gwarideni kila Ijumaa. Lengo ni kuamshia wanafunzi ari ya uanahabari na taaluma nyinginezo zinazofungamana na Kiswahili.

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: ALVINS KASUKU

CECIL ODONGO: Zipo dalili tele za mpasuko ndani ya One...

T L