Chama cha UDA chataka Babu Owino azimwe kushiriki uchaguzi wa Agosti 9

Chama cha UDA chataka Babu Owino azimwe kushiriki uchaguzi wa Agosti 9

NA CHARLES WASONGA

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) sasa kinaitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwaadhibu Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kuhusiana na jaribio la kuvuruga mkutano wa Kenya Kwanza katika uwanja wa Jacaranda, Nairobi, Jumapili.

Katika barua aliyoandikia tume hiyo, Katibu Mkuu wa chama hicho Bi Veronica Maina anadai kuwa polisi walitumiwa na chama cha ODM pamoja na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, kusababisha taharuki kwa lengo la kusambaratisha mkutano huo.

Bi Maina alisema kuwa mgombeaji ubunge wa Embakasi Mashariki kwa tiketi ya UDA Francis Mureithi ndiye alikuwa amekodi uwanja huo mnamo Juni 15 kwa kulipa Sh30,000 kwa serikali ya kaunti ya Nairobi.

“Lakini tunashangaa kuwa maafisa wa polisi waliziba njia za kuingia uwanja huo kuanzia asubuhi kwa madai kuwa Babu Owino pia alikuwa amekodi uwanja huo. Hii sio haki,” akasema.

Bi Maina sasa anaitaka IEBC kumzuia Bw Owino ili asishiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kwa kukiuka kanuni ya nidhamu hitajika wakati wa kampeni.

“Ni wajibu wa IEBC kumzuia Babu Owino kwa sababu kile kimetendeka leo katika uwanja wa Jacaranda kinaonyesha wazi kuwa mgombeaji huyu amekiuka kanuni hiyo na Katiba ya Kenya,” akaeleza.

Licha ya malalamishi kutoka kwa katibu huyu mkuu wa UDA, Naibu Rais William Ruto ambaye ni mgombea urais kwa tikiti ya chama hicho, aliwasifu maafisa wa polisi kwa kupambana na vijana waliotaka kuvuruga mkutano huo.

Aidha, aliwapongeza polisi kwa kupuuzilia mbali maagizo kutoka kwa wakubwa wao waliotaka mkutano huo utibuke.

“Tunawashukuru maafisa wetu wa polisi kwa kusimama kidete na kuhakikisha wamedumisha usalama hali ambayo imetuwezesha kufanya mkutano wetu. Hawa wangwana ni wazalendo ambao wanaelewa kuwa wajibu wao mkuu ni kudumisha amani,” akasema Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Akinyi na Kangangi wachupa uongozoni mbio za baiskeli za...

Mwamba RFC ni wafalme wa Driftwood 7s

T L