Makala

Chama cha ushirika kinavyotafutia wafugaji soko la maziwa

March 6th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU   

IKIWA kuna manufaa ambayo wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kaunti Ndogo ya Kieni Magharibi, Nyeri, wanajivunia ni kuungana kuanzisha chama cha ushirika.

Kieni Dairy Products Ltd ni muungano wa wakulima eneo hilo ambao umewafaa pakubwa kujiendeleza kimapato.

Shughuli za utendakazi zikiwa zilianza rasmi 2010, Afisa Mkuu Mtendaji, Solomon Maina anakiri wanachama wamenufaika kwa kiasi kikubwa kupanua mianya ya soko.

“Wazo kubuni muungano lilitujia 1995, na miaka 15 baadaye tukalizindua na tunajivunia hatua tulizopiga,” Maina anasema.

Chama hicho cha ushirika kina idadi jumla ya memba 6, 000, ambao ni wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Maziwa ni mojawapo ya mazao ya ufugaji ambayo kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakilalamikia bei duni.

Solomon Maina akionyesha yoghurt iliyoundwa na Kieni Dairy Products Ltd. PICHA|SAMMY WAWERU

Kuanzia kero ya kupunjwa na mabroka na mawakala hadi gharama ya juu ya uzalishaji maziwa, hawajakuwa na tabasamu kamwe.

Kulingana na Maina, bei ya chini ambayo wafugaji hulipwa lita moja ya maziwa ni Sh44 – suala linaloletea wanachama afueni.

Afisa huyu anadokeza kwamba Kieni Dairy Products Ltd inalenga masoko makuu, hasa viwanda vya kusindika maziwa.

“Ni daraja la kusaka masoko yenye ushindani mkuu ambalo sisi wenyewe kama wakulima tulijiundia,” anasisitiza.

Waziri wa Vyama vya Ushirika, Simon Chelugui, amekuwa akihimiza wakulima kuwa kwenye makundi au miungano ili kupata huduma za serikali kwa njia rahisi.

“Kwa mfano, mbolea ya bei nafuu wakulima walio kwenye miungano au vyama vya ushirika wanafikiwa na bidhaa bila vikwazo,” anasema.

Huduma hiyo ya fatalaiza ya bei nafuu iliyozinduliwa mapema 2023, wakulima wanaonufaika ni waliosajiliwa kidijitali.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali Dijitali, Maina alidokeza kwamba Kieni Dairy Products Ltd ni mojawapo ya maajenti wanaosambaza mbolea ya serikali kwa wakulima Kieni Magharibi.

Afisa Mkuu Mtendaji Kieni Dairy Products Ltd, Solomon Maina akipanga maziwa ya mtindi wakati wa maonyesho ya Sankalp Jijini Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Eneo hilo likiwa kati ya yanayoshuhudia ukame mara kwa mara, shirika hilo hutoa mafunzo kwa wafugaji jinsi ya kukuza malisho.

“Tuna programu za upanzi wa mseto wa nyasi zenye virutubisho, jinsi ya kujiundia malisho na kuyahifadhi kwa minajili ya msimu wa kiangazi,” akasema.

Kwa siku, muungano huo hukusanya zaidi ya lita 20, 000 za maziwa.

Huyachemsha, na kando na kulenga viwanda vikuu, huongeza thamani kwa kusindika maziwa ya mtindi – maarufu kama yoghurt.

Maziwa ya mtindi yaliyoundwa na Kieni Dairy Products Ltd. PICHA|SAMMY WAWERU

Chini ya nembo ya Highridge wana brandi mbili; Vanilla na Stroberi.

“Ikiwa kuna mtandao ambao tumebaini unateka pesa, ni kuongeza maziwa thamani,” Maina anasema.

Lita moja ya maziwa inapoongezwa thamani, afisa huyu anasema kiwango cha chini cha mapato inachoingiza ni Sh160 ishara kuwa mwanya huo ndio siri ya pesa.

Huku muungano huo ukiwa unatumia mashine za mikono (za zamani) kusindika maziwa, unaomba serikali kuusaidia kupata mitambo ya kisasa na ya kiotomatiki.

Kufuatia jitihada za muungano huo kuboresha sekta ya maziwa nchini, ilipata fursa kuhudhuria Makala ya 11 ya Sankalp Africa Summit 2024.

Solomon Maina, Afisa Mkuu Mtendaji Kieni Dairy Products Ltd akielezea mteja kuhusu huduma za chama hicho cha ushirika wakati wa maonyesho ya Sankalp Jijini Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Maonyesho hayo yaliyofanyika kati ya Februari 28 na 29, yalileta pamoja wafanyabiashara, wakulima, wajasirimali na wawekezaji kutoka sekta mbalimbali kuonyesha bidhaa na mazao yao.

Kieni Dairy Products Ltd ni miongoni mwa mashirika yanayonufaika kupitia miradi ya Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) na Sun Business Network (SBN).