Habari Mseto

Chama chadai BBI itahujumu mahakama

October 26th, 2020 1 min read

Na Charles Wasonga

CHAMA cha Justice and Freedom sasa kinataka ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) ifanyiwe marekebisho kabla ya kupitishwa ili kulinda uhuru wa Idara ya Mahakama na Bunge.

Kiongozi wa chama hicho Justus Juma haswa alisema pendekezo la kubuniwa kwa afisi ya mpokeaji malalamishi dhidi ya Majaji na Mahakimu ni sawa na kuingilia uhuru wa Idara ya Mahakama.

“Ikiwa mtu mmoja ataamua ikiwa Jaji anafaa kuondolewa au la, ina maana kuwa jaji huyo na wenzake watakuwa wakimwogopa na hivyo kupoteza uhuru wao wa kutoa maamuzi yao. Hii ni sawa na kuingilia uhuru wa idara ya mahakama kwa ujumla,” akasema jana kwenye kikao na wanahabari katika mkahawa wa Jukwaa Hotel, Nairobi.

Kulingana na ripoti ya BBI iliyozinduliwa rasmi jana wajibu wa mshikiliwa wa afisi hiyo atapokea na kuchunguza malalamishi dhidi ya majaji ambayo yatawasilishwa kwa Tume ya Huduma za Bunge (JSC).

Kwamba afisa huyo atateuliwa na Rais ndio sababu inayopelekea chama Justice and Freedom na wadau wengine kupinga pendekezo la kubuniwa kwa afisa hiyo.

“Kupitia kubuniwa kwa afisi hii jopokazi la BBI lililoongozwa na Seneta Yusuf Haji Idara ya Mahakama imegeuzwa kuwa sehemu ya Afisi ya Rais. Hii ina maana kuwa Rais ameangeza mamlaka hata zaidi ya ilivyo katika katiba ya sasa,” akasema Juma ambaye alikuwa ameandamana na katibu mkuu wa chama hicho Daniel Kwesi.