Habari Mseto

Chama chalia wanaume wanaopigwa na wake zao wasaidiwe

August 27th, 2019 1 min read

NA JOSEPH WANGUI

CHAMA cha Maendeleo ya Wanaume kimelia kwamba wanaume waliopo kwenye ndoa wanaendelea kupokezwa kipigo na wake zao, akisema serikali inafaa kuingilia suala hilo ili wanaotekeleza dhuluma hizo wakabiliwe kisheria.

Mwenyekiti wa chama hicho Nderitu Njoka alisema utafiti walioufanya miaka miwili iliyopita ilionyesha kwa saba kati ya wanaume 10 hunyoroshwa na wake zao na akasema kwa sasa idadi hiyo imepanda hata zaidi.

Bw Njoka pia aliomba serikali kukusanya data kuhusu dhuluma kwenye ndoa ili asasi za uchunguzi ziwachukulie hatua kali wanaoendeleza ukatili dhidi ya wapenzi wao.

“Wanaume ndio hudhulumiwa zaidi kwenye ndoa na hawasemi kwa hofu ya kuchekwa. Wale hupata majeraha ndio hujulikana kwa sababu hilo haliwezi kufichika. Idara ya mipango ya serikali inafaa kuwa na data inayoonyesha jinsi wapenzi wanavyodhulumiwa katika asasi za ndoa ili kuchukua hatua za kuwaokoa,” akasema Bw Njoka.

Afisa huyo pia aliwataka wanaume kuzinduka na kuanza kuripoti dhuluma wanazotendewa badala ya kuumia kimya kimywa kwenye ndoa zao.

Aidha alishikilia kwamba ndoa ni asasi muhimu lakini akaitaka afisi ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma(DPP) kuchunguza visa vya mwanandoa kumpiga na kumjeruhi mwenzake na kuwasilisha mashtaka dhidi ya wanaotekeleza ukatili huo mahakamani.

Bw Njoka pia aliiomba idara ya mipango ikusanye data kuhusu wajane na wanaume waliofiwa na wake zao ili wahusishwe kwenye mipango ya malipo ya serikali ndipo wafaidikie fedha hizo kama wakongwe.

“Watoto wa wajane hawaendelei na masomo kwa kukosa karo na vitabu. Serikali inafaa kuwa na taarifa kuhusu wajane ili kuwasaidia na pia kuwaokoa dhidi ya kudhulumiwa na watu wa ukoo wa waume wao,” akongeza Bw Njoka.