Chama chaomba mahakama itupilie mbali rufaa inayolenga kufufua BBI

Chama chaomba mahakama itupilie mbali rufaa inayolenga kufufua BBI

Na RICHARD MUNGUTI

CHAMA cha Thirdway Alliance kimeiomba Mahakama ya Juu itupilie mbali rufaa inayolenga kufufua mchakato wa kubadilisha katiba.

Chama hicho kilieleza Mahakama ya Juu kuwa mpango huo wa kubadilisha katiba uliongozwa na Rais Uhuru Kenyatta badala ya kushinikizwa na mapendekezo ya wananchi na haupasi kufufuliwa.

Kupitia kwa wakili wake, Bw Elias Mutuma, chama hicho kiliwasihi majaji wa Mahakama ya Juu wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, watupilie mbali rufaa zinazoomba mpango huo uzinduliwe tena na Katiba kufanyiwa mabadiliko kama ulivyozimwa na majaji saba wa Mahakama ya Rufaa na majaji watano wa Mahakama Kuu.

“Majaji hawa 12 waligundua makosa katika mchakato huo na kuzima juhudi za kubadilisha katiba wakisema ulikuwa na lengo la kuandika Katiba mpya,” Bw Mutuma alifafanunua.

“Naomba mahakama hii izime kabisa mpango wa kubadilisha katiba kwa vile uliongozwa na Rais Kenyatta badala ya kuzinduliwa kupitia maoni ya wananchi,” alisema Bw Mutuma.

Wakili huyo alisema Katiba imeeleza jinsi inavyoweza kubadilishwa na haijasema jinsi “inaweza kufutiliwa mbali au kuangamizwa.”

Wakili huyo alisema mchakato huo ulipotoka njia na kamwe haupasi kuidhinishwa na Mahakama ya Juu.

“Naomba mahakama hii ikubaliane na maamuzi ya majaji saba wa Mahakama ya Rufaa na wale watano wa Mahakama Kuu kwamba utaratibu uliofuatwa kuibadilisha katiba ulikinzana na sheria ,” alisema Bw Mutuma.

Alisema Katiba ya 2010 imeeleza utaratibu utakaofwatwa endapo mabadiliko yatafanywa.

Akinukunuu vifungu 88 ,255 na 257 vya Katiba , Bw Mutuma alisema ni wananchi tu wanaopasa kuzindua mabadiliko na wala sio Rais Kenyatta.

Aliongeza kuwa maoni ya wananchi hayakupokewa kama ilivyopendekezwa katika katiba .

Alisema sahihi milioni moja zilikusanywa na kupelekewa tume huru ya uchaguzi na mipaka (BBI) ndipo ikapeleka hoja kujadiliwa na mabunge ya kaunti.

Msimamo huo wa Thirdway uliungwa mkono na Miriru Waweru na Dkt Angela Mwikali kwamba mchakato wa kubadilisha katiba haukufuata sheria.

Kesi inaendelea.

  • Tags

You can share this post!

Mameneja 9 wa Kenya Power kortini kuhusiana na stima kupotea

Polisi wasaka wanaotupa miili Yala

T L