‘Kenya ingali inakabiliwa na changamoto za kuwapata madaktari bingwa wa mifugo na wanyama wa nyumbani’

‘Kenya ingali inakabiliwa na changamoto za kuwapata madaktari bingwa wa mifugo na wanyama wa nyumbani’

Na SAMMY WAWERU

OSCAR Ragui ambaye ni mfugaji hodari wa mbwa awali alikuwa akihangaika kupata soko.

Changamoto hiyo ilikuwa inaenda sambamba na ukosefu wa vetinari kuhudumia mifugo wake.

Anakumbuka kisa ambapo 2019 alipoteza watoto kadhaa wa mbwa, anaosisitiza endapo wangefanikiwa kuwa hai wangemuingizia kitita cha kuridhisha cha pesa.

Walikufa kutokana na maradhi ya Parvovirus.

“Kupata daktari wa mifugo, hasa anayeshughulikia masuala ya mbwa haikuwa rahisi,” Oscar asema.

Vilevile, hufuga ng’ombe wa maziwa na anaelezea kwamba mahangaiko ya mbwa ni sawa na mifugo hiyo kupata vetinari.

Kero hiyo haswa inatokana na sekta ya mifugo nchini kusheheni maafisa na mavetinari bandia.

Serikali inakiri suala hilo ni changamoto kuu, ikiendelea kuimarisha mikakati kuboresha sekta hiyo.

“Kwa sasa, tuna inspekta mmoja katika kila kaunti anayesaidia kukabili kuwepo kwa maafisa bandia wa mifugo,” anasema Katibu katika Wizara ya Mifugo, Bw Harry Kimtai.

Dkt Lucy Jeptepkeny, ambaye ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa Kaunti ya Uasin-Gishu na Kajiado, ni kati ya waathiriwa wa kero ya mavetinari ghushi.

“Mwaka wa 2014 na 2020 nilipoteza ng’ombe wawili wenye thamani zaidi ya Sh430, 000 kupitia maafisa bandia,” Dkt Lucy akumbuka, akikadiria hasara.

Kufuatia hasara iliyomfika, mfugaji huyo alikata kauli kuwekea mifugo wake bima.

Bodi ya Huduma za Mifugo Nchini (KVB), inahimiza wafugaji kushirikiana nayo ili kung’oa ‘maafisa’ wahuni.

Inasema, ni muhimu mfugaji kuthibitisha ikiwa vetinari anayehudumia mifugo wake amesajiliwa na kuidhinishwa na KVB.

Bodi hiyo yenye makao yake makuu Kabete, Kaunti ya Kiambu, ni taasisi ya serikali.

Licha ya pandashuka hizo, ambazo Oscar Ragui hakuziepuka wakati akiwa limbukizi katika ufugaji, anasema soko pia ni miongoni mwazo.

Huku mradi wake ukiwa ni wa kujamiisha na kuzalisha mbwa wa ulinzi, mabroka walikuwa wakimkaba koo wakati wa kuingia sokoni.

Hilo hasa linatokana na miundomsingi duni na mbovu ya soko Kenya, ambayo inazingira kila mkulima na mfugaji.

Mabroka almaarufu mawakala, ni wafanyabiashara wanaounda faida mara dufu kupitia mazao ya kilimo na ufugaji, kwa madai ya kuwatafutia wanunuzi.

Wameteka nyara masoko, mwanya ambao wanautumia kukandamiza wanazaraa na wafugaji bila huruma.

“Kabla nifumbue macho, walinivuna hela sawasawa,” Oscar asema.

Hata hivyo, kwa sasa anahoji wanamuonea kwenye ‘kioo’.

Kwa vyovyote vile hatangamani nao, akisifia programu aliyovumbua.

Maarufu kama Bobbi, ni apu inayomsaidia kupata wanunuzi wa vilebu wake (wana wa mbwa) na pia mazao ya ng’ombe anaofuga – maziwa.

Isitoshe, mtandao huo kando na kuondoa mabroka, unamuunganisha na mavetinari mifugo wake wanapougua au anapohitaji ushauri nasaha.

“Wanachotaka wakulima na wafugaji, ni miundomsingi hususan ya soko iimarishwe ili kuwanusuru kutoka vinywa vya mawakala,” Oscar afafanua, akidokeza wakulima na wafugaji wenza waliojisajili na apu yake wanaendelea kuridhia huduma bora.

Wakulima na wafugaji wengi wamejipata kuasi miradi waliyowekeza, kwa sababu ya kero ya soko.

Gharama ya juu ya pembejeo na malisho ya mifugo, pia imechangia kutatiza utendakazi wao.

Miundomsingi ya soko ikiboreshwa, waweze kutia kibindoni mapato ya kuridhisha itakuwa rahisi kujiendeleza kimaisha.

Takwimu za utafiti wa Ubalozi wa Denmark Kenya mwaka uliopita, zinaonyesha janga la Covid-19 limesababisha wengi kuingilia shughuli za ufugaji na kilimo.

“Sekta ya Kilimo na Ufugaji Kenya inaendelea kuimarika,” anasema Bw Charles Wasike, Meneja Msimamizi wa Mikakati katika ubalozi huo kitengo cha kilimo-biashara na bunifu kuangazia mabadiliko ya tabianchi.

Athari za virusi vya corona, zimechangia watu wengi kupoteza ajira za ofisini wengi wao wakikumbatia ukulima na ufugaji kujiendeleza kimaisha.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Alumirah aahidi kuiongoza Harambee Starlets kufuzu...

AFCON: Wanane waaga dunia baada ya mkanyagano wa mashabiki...

T L