Changamoto tele zinazomsubiri Biden kukabili

Changamoto tele zinazomsubiri Biden kukabili

Na AFP

JOE Biden jana aliapishwa rais wa 46 wa Amerika na kutamatisha utawala wa Donald Trump uliosheheni misukosuko na migawanyiko.Biden sasa anaanza kibarua kigumu cha kupambana na janga Covid-19 na kupalilia umoja katika taifa lililogawanyika chini ya uongozi wa Trump.

Biden, 78, ambaye alikuwa makamu wa rais kwa miaka minane chini ya utawala wa Barack Obama, na seneta kwa muda mrefu wa Delaware, aliapishwa saa 12 jioni jana (saa sita saa za Amerika) nje ya jengo la Capitol, jijini Washington.

Japo shughuli ya kupitishwa kwa mamlaka ilifanyika ilivyo kawaida kwa zaidi ya karne mbili, hafla ya jana ilikuwa ya aina yake.Zaidi ya maafisa 25,000 ya usalama, wakiwemo wanajeshi, walimwagwa jijini Washington kwa ajili ya kuzuia fujo za Januari 6 za jaribio la Trump kupindua serikali.

Raia wa kawaida walizuiwa kuhudhuria shughuli hiyo ya kuapishwa kwa Biden kutokana na janga la Covid-19.Alipowasili Washington Jumanne, Rais huyo mpya alitoa risala maalum kwa zaidi ya watu 400,000 ambao wameangamizwa na janga hilo kufikia sasa.Biden vile vile alikariri kujitolea kwake kuunganisha taifa la Amerika baada ya fujo zilizosababishwa na Trump.

Kawaida umati mkubwa wa watu hukusanyika jijini Washington siku moja kabla ya kuapishwa kwa rais mpya.Lakini Biden ambaye aliandamana na Makama wa Rais Kamala Harris walikuwa pekee yao katika ukumbi huo.Badala yake bendera 200,000 ziliwekwa kuwakilisha umati wa watu ambao haukuwepo.

Mnamo Jamanne, Trump, ambaye hajaonekana hadharani kwa wiki moja, alivunja kimya chake kwa kuhutubia taifa kwa njia ya video, na kwa mara ya kwanza aliwataka Waamerika “kuombea” ufanisi wa utawala mpya.\Trump hajawahi kumpongeza rais huyo mpya kufuatia ushindi wake.

Kazi ya mwisho aliyofanya jana kabla ya kupanda ndege kuelekea nyumbani kwake jimbo la Florida ni kutoa msamaha kwa watu 73 waliohukumiwa kwa makosa mbalimbali au wanakabiliwa na mashtaka.

Miongoni mwao ni wandani wake wakuu.Mmoja wa washirika wake waliofaidi kutoka na msamaha huo ni Steve Bannon, aliyeshtakiwa kwa kuiba pesa zilizochangwa kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kati ya mpaka wa Amerika na Mexico.

Hata hivyo, orodha hiyo iliyotolewa na Ikulu ya White House haikuwa na jina la Trump au jamaa zake. Awali, taharuki ilitanda katika Capitol Hill ambako Seneti ilitarajiwa kujadili mashtaka dhidi ya Trump baada ya Bunge la Wawakilishi kupitisha kura ya kumng’oa mamlakani kwa kuchochea fujo za Januari 6.

Rais Biden anatarajiwa kuwasilisha orodha ya watu aliowateua katika baraza lake la mawaziri waidhinishwe.

You can share this post!

MWISHO WA GIZA!

Vyama vipya vinaundwa kwa misingi ya ukabila – Msajili