Changamoto za kiufundi zachelewesha mpango wa kadi za kielektroniki kwa wavuvi

Changamoto za kiufundi zachelewesha mpango wa kadi za kielektroniki kwa wavuvi

Na KALUME KAZUNGU

MASWALI yameibuka baada ya kubainika kuwa mpango wa serikali kuwapa wavuvi wa Kaunti ya Lamu vitambulisho maalumu vya kidijitali haujatekelezwa miaka mitatu baada ya kuzinduliwa.

Kadi hiyo inayofahamika kama ‘Mvuvi Card’ ilinuiwa kusaidia kuzuia magaidi kuingia katika bahari za Kenya wakijifanya kuwa ni wavuvi.

“Walitushirikisha kwenye mpango huo. Tukaukaribisha kwa mikono miwili. Walitupiga picha. Pia walichukua majina yetu, nambari za vitamblisho na maelezo mengine waliyotaka kujumuisha kwenye kadi hiyo. Kilichosalia ilikuwa ni kungoja kadi. Tunashangaa kwamba miaka inasonga na hakuna aliyepewa kadi hiyo maalum. Serikali itujulishe ikiwa mpango huo bado upo ama waliukatiza,” akasema Mwenyekiti wa Vyama vya Ushirika wa Wavuvi (BMU) tawi la Lamu, Mohamed Somo.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alikiri kwamba mpango huo haujatekelezwa lakini akataka wavuvi wawe na subira.

“Kumekuwa na changamoto za kiufundi katika kuandaa vitambulisho hivyo. Tuko kwenye harakati za kutatua changamoto hiyo. Wavuvi wasiwe na shaka. Wajue mpango bado upo,” akasema Bw Macharia.

Katibu wa wavuvi wa kisiwa cha Lamu, Abubakar Twalib, alisema walitazamia mpango huo ungesaidia kusitisha hofu ambayo wavuvi wamekuwa nayo kila wakati wanapovua samaki baharini hasa nyakati za usiku.

Kwa kipindi kirefu wavuvi wa Lamu hawajakuwa wakitekeleza uvuvi wa usiku baharini kwa sababu za kiusalama.

Mnamo Mei, 2019 wakati Waziri wa Usalama wa ndani, Fred Matiang’i alipozuru Lamu, aliamuru marufuku ya kuvua usiku kuondolewa kote Lamu.

Baadhi ya wavuvi wa Lamu awali wakisajiliwa kupewa kadi maalum za kielektroniki. Ni miaka minne sasa na hakuna mvuvi hata mmoja wa Lamu ambaye amepokea kadi hiyo. Picha/ Kalume Kazungu

Pia aliamuru wavuvi wote kusajiliwa kwa njia ya kielektroniki ili iwe rahisi kwao kutambuliwa na walinda usalama wanapotekeleza shughuli baharini.

Bw Twalib alisema endapo mpango wa kuwapa Mvuvi Card utatimizwa, wavuvi wengi, ikiwemo wale ambao awali walisitisha shughuli kwa kuogopa kuteswa na walinda usalama baharini wangekuwa wamerejelea kazi zao, hatua ambayo ingeboresha sekta ya uvuvi kwa jumla.

You can share this post!

Serikali yafanya ukaguzi wa shule Nakuru

Tujipange la sivyo tutapangwa, Kabogo ahimiza Mlima Kenya