Makala

Changamoto za mji wa Nakuru katika azma ya kuwa jiji

September 15th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Miundomsingi duni inazidi kulemaza azma ya Kaunti ya Nakuru kupata hadhi ya kuwa jiji kuu ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Wakazi wa mitaa ya Barut, Shabbab, Kaptembwa, Rhonda, Freearea na London bado wanakabiliana na changamato za uzoaji taka, makazi duni, ukosefu wa maji safi na hali mbaya ya barabara zenye mashimo.

Mnano 2018 serikali ilitoa kima cha bilioni 1.9 kuboresha barabara za mijini na mashinani,ikiwa ni mojawapo ya ajenda kuu kuboresha miundo msingi, ambayo ni ya kutiliwa shaka.

Kulingana na bwana Silas Kinoti kutoka KURA(Kenya Urban Roads Authority), hatua hiyo ilikuwa ni sehemu ya mradi wa serikali kutengeneza kilomita 137,mradi uliogharimu bilioni 9.8.

Ongezeko la idadi ya vijana wanaohamia mijini wasiokuwa na ajira ikiwa ndilo pigo jingine, huku magenge kadhaa yakiibuka mengi yakihusishwa na viongozi.

Brian Wabwire mkaazi wa Pondamali anasema kuwa ni kama baadhi ya mitaa ya mabanda imetengwa na serikali ya kaunti na wala haina nafasi katika mipango ya serikali.

Kulingana naye haoni haja ya Nakuru kupata hadhi ya kuwa jiji kuu, ilhali pengo kati ya matajiri na maskini ni kubwa.

Anapendekeza kuwa serikali iwashughulikie kwanza raia wake,kwa kufufua viwanda na kubuni nafasi za ajira kama njia ya kutimiza ahadi yao wakati wa kampeni za 2017.

Wambire anaona Nakuru kuwa jiji kuu itakuja na hasara nyingi kuliko faida,kwani tayari wamiliki wa nyumba wamepandisha kodi na kufanya maeneo ya kufanyia biashara kuwa nyumba za kukodisha.

Ongezeko la taasisi za kutoa elimu kwa wanafunzi wa vyuo na taasisi za kiufundi, ikiongeza ushindani kwa makazi haba yanayopatikana Nakuru.

“Kwanza serikali iwekeze katika ukarabati wa miundo misingi kama daraja za wapita njia na makazi ya bei nafuu,” akasema.

Serikali irekebishe mikondo ya kupitiza maji, inayofurika hasa msimu wa mvua,na kusababisha uharibifu wa mali.

Alitoa mfano wa barabara ya Rhonda ambayo haipitiki, na biashara zimesimama tangu wiki iliyopita.

Mvua ilisomba mali za watu na kuwajeruhi wengine,maji yalipozidi na kuvunja kingo zake

Ingawa KENHA walitembelea eneo hilo na kuahidi wakazi kuwa wangekarabati upya maeneo yao ya kufanyia biashara,bado hawajawajibika.

Gilbert Kamau mwendeshaji boda pia anapendekeza watengewe sehemu ya kupokea abiria na kupakia pikipiki zao.

Kamau anasema baraza la usimamizi wa mji Kanjo wamekuwa wakiwahangaisha kwa kufanya misako ya mara kwa mara na kuwapokonya pikipiki zao wanaposhindwa kulipia faini.

Aidha sehemu za kupakia pikipiki zinazopatikana katika kaunti ya Nakuru ni haba, ambapo wengi wao wamekuwa wakilaumiwa kwa msongamano wa magari ukitatiza uchukuzi.

“Tungependelea kuona ushirikiano baina ya KERRA, KURA na KEnHA na pengine benki ya dunia, kutumia nafasi zinazopatikana kwa faida ya vijana,”alisema.

Vilevile baadhi ya wakazi wanasema kaunti haijajiandaa vilivyo kukabiliana na mikasa ya moto, na majanga ya kitaifa kwa mfano shughuli ya uokozi katika ziwa Nakuru mwaka uliopita ilichukua muda mrefu kuwaokoa manusura.

“Ambapo mpaka sasa baadhi ya familia hazikuwapata wapendwa wao ili waweze kuwazika,”Kamau aliongezea.

Hii ndio sababu tangu awamu ya uongozi wa Gavana Lee Kinyanjui alianzisha mchakato wa BORESHA BARABARA, uliopania kupanua njia zinazoweza kupitika.

Alikusudia kuongeza idadi ya barabara na kuwarahisishia wafanyibiashara wanaotumia njia kuu kusafirisha bidhaa zao hadi sokoni.

Katika ajenda zake gavana Lee alihakikisha kuwa barabara katika wadi 55 zinazozunguka kaunti ya Nakuru zitapatiwa kipaumbele.

Gavana Lee Kinyanjui akiwahutubia wakazi wa Nakuru katika ajenda yake moja alianzisha mradi aliobatiza jina BORESHA BARABARA. Picha/ Richard Maosi

Alibuni jopo kazi la kuangazia maegesho,kukabiliana na majanga, kukarabati miundo msingi iliyoharibika na

kwa kushirikisha wafadhili wa kimataifa kama vile benki ya dunia.

Mhandisi John Otiato kutoka KURA anasema raia wengi ndio wa kulaumiwa kwa kufanya shughuli zao hadi katika maeneo yaliyotengewa kuwa barabara.

“Wakazi wengine wamekuwa wakitekeleza kilimo kando ya njia na wamekuwa wakiandamana kila mara serikali inapojaribu kuwatimua,” akasema.

Aliongezea kuwa wakati mwingine imekuwa vigumu kupata vyombo vya kutengenezea barabara, ikiaminika kuwa kaunti imepandisha bei ya mchangarawe na simiti.

Wakati mwingine gharama huwa zaidi ya mara tatu ya ile bei iliyozoeleka .