Dondoo

Changudoa atimuliwa kwa kuanika chupi hadharani kuteka waume

September 11th, 2018 1 min read

Na CHARLES ONGADI

Mtwapa, Kilifi

AKINA mama waliojawa na hasira za mkizi walimtimua changudoa mpangaji mwenzao kwa tabia ya kuanika chupi zake hadharani.

Kwa mujibu wa mdokezi, akina mama hao walidai kipusa huyo alifanya hivyo akilenga kuteka hisia za waume wao.

“Hii tabia ya mwanamke huyu kutuanikia chupi zake mbele ya milango yetu ni uchokozi na ni lazima ahame hapa apende asipende,” mama mmoja alisikika akimnong’onezea mwenzake kwa hasira.

Kufumba na kufumbua, akina mama hao walikusanyika katika veranda na kumbishia kipusa huyo aliyekuwa akijipodoa chumbani mwake akijitayarisha kwa mishemishe zake za siku.

Akina mama hao walimtaka kuondoa mara moja chupi zake zote alizoanika kwenye kamba iliyokuwa verandani na kufunganya virago vyake kuondoka ploti hiyo au aone cha mtema kuni.

“Kwani nia yako ni gani wewe ? Wataka kutuibia waume wetu kwa kuwachochea kwa chupi zako, ondoka ama tukuoneshe kivumbi,” alibweka mama mmoja kwa hasira.

Walidai kwamba mbali na mwanadada huyo kuanika chupi zake hadharani pia alikuwa na mtindo wa kuvalia nguo zisizo za heshima na kuchukua muda mwingi akiongea na kutaniana na waume wao.

Licha ya kipusa kujitetea kwamba alikuwa akianika chupi zake ili zipate kukauka haraka na wala hakuwa na nia yoyote mbaya, akina mama hao hawakutaka kusikia la mwadhini wala mteka maji msikitini.

Na kwa kuwa wengi wape, alisalimu amri na kuomba kupewa muda kutafuta nyumba kwingine ahame.

Lakini alipokuwa akihama, aliapa kuwafunza akina mama hao adabu kwa kumsingizia na kumfukuza.

“Hao mnaowaita waume wenu watanitafuta wenyewe basi mpende msipende na hadi mnikome nyie,” alisema kwa hasira.