Michezo

Chania High yatisha kwa karate

June 6th, 2024 2 min read

NA LAWRENCE ONGARO

SHULE ya Upili ya Chania High mjini Thika inafahamika kwa kuruhusu wanafunzi kushiriki michezo tofauti.

Baadhi ya michezo ambayo wanafunzi wanajihusisha sana nayo shuleni humo ni soka, voliboli, handiboli, vikapu, raga na mashindano ya uogeleaji.

Lakini pia mchezo wa karate shuleni humo umewavutia wanakarate 50.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw James Gitau, anasema kuwa kwa zaidi ya miaka mitano ambayo amekuwa katika shule hiyo, amezingatia mambo mawili muhimu ambayo ni masomo na michezo.

“Mambo hayo mawili yameiweka shule hiyo katika ramani nchini ambapo wanafunzi wanapata gredi nzuri huku wakitia fora michezoni,” alisema Bw Gitau.

Wakufunzi wawili ambao wamejitolea kunoa vijana wa karate shuleni humo ni Jediel Mutua na Samuel Mutiga ambao wameiweka shule ya Chania high katika mstari wa mbele  katika mchezo huo.

Kocha Samuel Mutiga (kushoto) na Jediel Mutua wakionyesha cheti maalum ambacho Chania High ilituzwa baada ya wanafunzi wanaoshiriki mchezo huo kufanya vyema katika mashindano. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Bw Mutiga anasema wanakarate (karateka) wake wamejitolea mhanga kuona ya kwamba wanatamba katika mashindano yajayo.

Mnamo Juni 8 na Juni 9, 2024, wanakarate wa Chania High watashiriki katika mashindano ya karate kwa chipukizi ambayo yanawaleta pamoja washiriki kutoka shule za eneo la Mlima Kenya. Yataandaliwa katika ukumbi wa Pastoral Centre mjini Thika.

Mwalimu mkuu wa Chania alisema shule hiyo imechukua jukumu la kununua vifaa vyote vinavyostahili vya michezo yote maarufu bila kubagua.

“Hatua hiyo imewapa wanamichezo motisha ya kujizatiti kufanya vyema michezoni.

Mkufunzi Mutiga alisema kuwa mazoezi ya karate hufanyika kila Jumatatu, Jumanne na Ijumaa kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa moja jioni.

“Wengi wa vijana wangu ninawanoa ili kujitayarisha pia kupandishwa gredi za kijani kibichi na manjano ili waweze kupanda katika viwango vingine vya juu,” alisema kocha huyo.

Bw Gitau kwa upande wake aliwatia shime huku akipongeza juhudi za wanakarate hao kujiunga na mchezo huo.

Alisema wanafunzi wake wanaoshiriki mchezo huo huonyesha nidhamu ya hali ya juu.

“Karate husaidia wachezaji kuimarisha mienendo yao,” alisema Bw Gitau.

Alisema kwenye matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023), shule ya Chania High ilikuwa miongoni mwa shule 10-bora katika kaunti nzima ya Kiambu.

Hivi majuzi katika mchezo wa karate uliofanyika mjini Thika, vijana chipukizi wa Chania High walionyesha ubora wao na kuzoa medali kadha.

Bw Gitau aliahidi kwamba atahakikisha wachezaji wa karate katika shule hiyo wanapata ukumbi mkubwa wa kufanyia mazoezi yao.