Michezo

Chapa Dimba ilivyomfungulia David Majak milango ya heri

September 11th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

DAVID Majak, 20, ambaye ni matunda ya michezo ya Chapa Dimba na Safaricom Season One ameibuka chipukizi wa hivi karibuni kushiriki mechi za kimataifa.

Chipukizi huyo alibahatika kuwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha taifa cha Sudan Kusini waliocheza dhidi ya Equatorial Guinea kwenye mechi ya mkumbo wa kwanza kuwania tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 iliyopigiwa Al-Hilal Stadium, Omdurman Sudan mapema mwezi huu.

Licha ya kushiriki patashika hiyo ndani ya dakika 54 pekee, aliiwezesha Sudan Kusini kutoka sare ya bao 1-1. Kwa mara nyingine mchana nyavu huyo anatazamiwa kushirikishwa katika kikosi hicho kwenye mchezo wa marudiano utakaochezewa jijini Malabo, Equatorial Guinea Jumapili ijayo.

Katika mashindano ya Chapa Dimba na Safaricom Season One, alisaidia Kapenguria Heroes kubeba taji la kitaifa katika fainali zilizochezewa Bukhungu Stadium, Kakamega. Kwenye michuano hiyo alionyesha mchezo safi na kubahatika kutwaa tuzo ya mchezaji anayeimarika (MVP).

Baada ya mafanikio hayo Tusker FC ilitwaa huduma zake kuichezea kwenye mbio za Ligi Kuu msimu uliyopita (2018-2019) ambapo aliitingia magoli sita na kuisadia kumaliza ya nne kwenye jedwali.

Mchezaji huyo aliendelea kupaisha mchezo wake hali iliyofanya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Nchini (SJAK) kumteua kuwania tuzo ya chipukizi bora mpya.

Tuzo hiyo iliwaniwa na wachezaji wafuatao: David Majak (Tusker), Joshua Otieno (SoNy Sugar), Nixon Omondi (Kariobangi Sharks), Daniel Sakari (Kakamega Homeboyz), Moses Mudavadi (Bandari) na Jackson Dwang (Nzoia Sugar).