Bambika

Charlene Ruto ateuliwa balozi wa damu baada ya kunyamazia suala la ikiwa Daddy Owen ni wake damu damu

January 19th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Afya Susan Nakhumicha, amemteua bintiye Rais William Ruto, Charlene Ruto, kuwa Balozi wa Damu nchini.

Kwenye barua iliyoandikwa Desemba 14, 2023, Bi Nakhumicha alisifia mchango wa Charlene kwenye harakati za utoaji damu nchini.

“Wizara ya Afya inakutambua na kukushukuru sana kwa mchango wako nchini kupitia utoaji damu, kuishinikiza, kuielimisha na kuihamasisha familia yako, jamii, marafiki wako na Wakenya kwa ujumla kujihusisha kwenye utoaji wa damu,” ikaeleza barua hiyo.

Waziri pia alimshukuru Charlene kwa juhudi ambazo amekuwa akiendesha kuchangisha pesa ili kufadhili shughuli za utoaji damu.

“Barua hii ni ya kukuteua kama Balozi wa Damu Kenya na kukuomba kwamba: endelea kuwa msemaji kwa marafiki wako, Vijana wa Kenya na raia wote,” ikaongeza barua hiyo.

Pia, aliraiwa kuwahamasisha watu kujitolea kutoa damu ili kuokoa maisha. Zaidi ya hayo, aliombwa kushirikiana na Mamlaka ya Kusimamia Ubadilishanaji wa Viungo vya Mwili Kenya (KTTA).

Kutokana na uteuzi huo, Charlene pia alipewa jukumu la kushirikiana na wahisani wengine katika masuala yanayohusiana na utoaji damu, kuandaa vikao vya kuuelimisha umma kuhusu utoaji damu na kuchangisha fedha za kufadhili shughuli hizo.

Charlene, 31, ndiye mtoto wa Rais Ruto ambaye amekuwa akionekana sana katika masuala yanayohusu raia.

Baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa mwonekano wake ni njia ya kujijenga ili kuwania nafasi ya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu ujao, jambo ambalo amelikanusha mara kadhaa.

“Lengo langu ni kuwa sauti kwa vijana na kuwasaidia raia,” akasema.

Wadaku wa safu ya burudani waliingiwa na uvumi kwamba Charlene na mwanamuziki Daddy Owen walikuwa na uvutio wa uchumba baada ya kutembelea wazazi wa kidume katika Kaunti ya Kakamega mwishoni mwa Desemba 2023.

Wawili  hao walinyamazia stori hiyo, ambapo kufikia sasa, wangali wamewaacha wadaku na alama za dukuduku.

Msanii Daddy Owen akiwa na Bi Charlene Ruto. PICHA | HISANI

Ngoma, semi, miondoko na utani kati yao, vyote viliwaangazia kama waliokuwa wamefika awamu ya mapenzi ambapo kama kikohozi, hayafichiki eti.

“Lakini naomba tusifike huko, sio kila mara wawili wakionekana pamoja inakuwa ni kasheshe…nimekuwa katika haya mambo ya usanii kwa miaka 20 sasa…sisi ni marafiki wa kufaana lakini hayo mengine kwa sasa tuyakome,” akasema Owen ambaye jina lake kamili ni Owen Mwaita.

Katika mitandao yake ya kijamii Owen amekuwa akishikilia kwamba uhusiano wake na Charlene ni ule wa kuwafaa waja mashinani na miradi mingine ya usanii.

Mnamo siku ya Krismasi, wawili hao walionekana katika vituo vya matatu wakitoa zawadi na tuzo nyingine haswa kwa vijana.

Hata hivyo, mchekeshaji Eddie Butita alimshauri Owen kwamba iwapo itafika awamu ya mapenzi, achukue tahadhari kwa kuwa “hata mkikosana na Charlene, msimamo wako na maoni yako hayatakuwa na maana kwa kuwa utakuwa wa kupangwa”.

Soma Pia: Eddie Butita: Ukitafuta mapenzi kwa familia ‘high-class’ simu yako inanuswa