Makala

Charlene Ruto: Nataka mume atakayenisaidia kuhudumia vijana

February 26th, 2024 2 min read

FRIDAH OKACHI na MWANGI MUIRURI

BINTIYE Rais William Ruto, Charlene Ruto ametangaza kwamba anatamani sana kupata mume atakayemsaidia kuafikia maono yake katika huduma zake kwa vijana nchini.

Bi Charlene, alitoa tangazo hilo mnamo Jumapili, Februari 25, 2024 ambapo alimsihi Pasta tajika, Benny Hinn kumuombea apate mume atakayemuunga mkono katika azma yake.

Mchungaji Benny amekuwa nchini kwa muda wa siku mbili mfululizo, ambapo aliongoza hafla ya maombi ya uponyaji kwa taifa katika Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi.

Mkutano wa mhubiri huyo ulihudhuriwa na mkewe Rais Ruto, Mama wa Taifa, Bi Rachael Ruto, mke wa naibu rais – Rigathi Gachagua, Pasta Dorcas Gachagua, kati ya wahubiri, na viongozi na wanasiasa mashuhuri nchioni.

Rais na naibu wake pia waliuhudhuria mnamo Jumapili, na wakati wa awamu ya maombi Bi Charlene alisema angetaka kupata mume atakayeunga mkono ndoto zake kwa vijana.

Bintiye Rais alijitambulisha kwa kuelezea jinsi anapenda sana vijana wa Kenya na Africa, akihoji Mungu amemteua kuwahudumia.

“Naomba Mungu aniundie njia niweze kuafikia mapenzi yake kwa vijana,” alisema.

Pasta Benny, aliomba waliokuwa kwenye mkutano huo kusimama.

Wazazi wa Charlene; Rais Ruto na Bi Rachel Ruto walishuhudia mhubiri huyo akimzunguka Charlene mara saba, kwa nyimbo na maneno ya kuthibitisha.

Mchungaji Benny aliomba akimtakia Baraka apate mume aliyetamani.

Aidha, Mtumishi huyo alimwomba Mungu ampe Charlene mume atakayemuunga mkono hivi karibuni.

“Mungu, mpe mume ambaye atatimiza wito huo pamoja naye. Tuma mwanamume katika njia zake. Hii itampa nguvu na kuwa msaada mkubwa kwake. Hawezi kufanya hivi peke yake Bwana, anaenda kwenye uwanja wa vita ili kunyakua kambi ya adui,” aliomba Pasta Benny.

“Anahitaji mume Bwana, na anamhitaji huyo mume haraka, mtume haraka. Wacha awe vile yeye anataka, kila kitu anachotaka kuhusu mume, mpe Bwana,” aliendelea Mchungaji.

Ombi la Bi Charlene, lilionekana kuwa kinaya ikizingatiwa kuwa miezi michache iliyopita alizuru nyumbani kwa msanii tajika wa injili, Daddy Owen, duru zikiarifu wawili hao ni wapenzi.

Wakati wa ombi hilo, Rais Ruto na Bi Rachel walionekana wakicheka huku Pasta Benny Hinn akimwambia Charlene aende akamchukue.