CHARLES WASONGA: Bei ya Sh3,500 ya mbolea si afueni tosha kwa wakulima

CHARLES WASONGA: Bei ya Sh3,500 ya mbolea si afueni tosha kwa wakulima

TANGAZO la Rais William Ruto kwamba wiki hii wakulima wataanza kununua mbolea kwa bei ya Sh3,500 badala ile ya awali ya Sh6,500 kwa gunia la kilo 50, lilipokelewa kwa furaha.

Akihutubia taifa baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya, Dkt Ruto alisema tani 1.4 milioni za mbolea zitawasili nchini na kusambaziwa wakulima kote nchini kwa bei hiyo nafuu.

Alisema mpango huo wa utoaji mbolea kwa bei nafuu utawafaidi wakulima wa mimea ya chakula msimu huu wa mvua fupi (Septemba hadi Desemba).

Aina ya mbolea ambayo Dkt Ruto alikuwa akirejelea ni ile inayojulikana kama Diamonium Phosphate (DAP), ambayo hutumika kwa wingi kupanda nafaka.

Lakini Rais Ruto alichelea kusema lolote kuhusu ruzuku ya mbolea ambayo ilianzishwa na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta kwa kima cha Sh5.7 bilioni.Chini ya mpango huo ambao ulitangazwa na Waziri wa Kilimo anayeondoka Peter Munya mnamo Aprili 15, 2022, mbolea ya DAP ingeuzwa Sh2,800 kwa gunia la kilo 50.

Nayo mbolea aina ya NPK ingeuzwa Sh3,000, MOP (Sh2,500), CAN (Sh1,950), Urea (Sh2,700) na Sulphate of Ammonia (Sh2,500).Katika mpango huo ambao haujasitishwa (sawa na ruzuku ya unga wa mahindi), kila mkulima huruhusiwa tu kununua magunia 20 ya mbolea kwa wakati mmoja.

Lakini wakulima wa mashamba makubwa walilalamikia sharti hilo, wakisema hatua ya kudhibiti idadi ya magunia wanayoruhusiwa kununua si sawa.Itakumbukwa kwamba wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022, Dkt Ruto na wandani wake katika Kenya Kwanza waliahidi kupunguza bei ya mbolea hadi Sh2,500 iwapo wangeibuka washindi na kuunda serikali.

Chini ya kivuli hicho, bei mpya ya Sh3,500 ambayo Rais Ruto alitangaza wiki jana katika uwanja wa Kasarani ingali juu, ikilinganishwa na Sh2,800 iliyotangazwa na serikali ya Jubilee mnamo Aprili 15 na Sh2,500 ambayo Dkt Ruto aliahidi wakati wa kampeni.

Hivyo, bei mpya haitatoa afueni kwa wakulima na wananchi kwa misingi ya matarajio yao.

Isitoshe, haitawafaidi wakulima kutoka maeneo ya North Rift, kama Trans Nzoia na Uasin Gishu, kunakokuzwa nafaka kwa wingi hususan mahindi.

Msimu wa upanzi maeneo hayo huanza Februari hadi Aprili, kipindi ambacho mbolea ya upanzi DAP iliuzwa kati ya Sh4,500 na Sh5,500 kwa kila gunia la kilo 50.

Serikali iwekeze katika ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza mbolea humu nchini badala ya kutegemea mataifa ya ng’ambo. Ni kwa njia hiyo ambapo tutapata mbolea ya bei nafuu siku zote. kwa kipindi kirefu kwa manufaa ya wakulima

Bei hii mpya itafaidi wakulima kutoka maeneo ambako wakulima hupanda mahindi mara mbili kwa mwaka haswa maeneo ya Nyanza na Magharibi mwa Kenya.

Bila shaka mpango huu utatoa afueni kwa wakulima wa janibu hizo ila mashamba yao ni madogo na hukuza mahindi kwa ajili ya matumizi nyumba sio kuuzwa kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

Ushauri wangu kwa serikali ya Dkt Ruto ni huu: Isitishe mpango wa uagizaji mbolea kutoka mataifa ya Urusi, Ukraine na mengine ya bara Uropa. Badala yake iagizae bidhaa hiyo kutoka nchi kama Morocco ambayo huizalishwa kwa wingi.

Pili, serikali ya Kenya Kwanza iwekeze fedha katika mpango wa utengenezaji wa kiwanda cha kutengeneza mbolea humu nchini badala ya kutegemea mataifa ya ng’ambo.

Mipango kama hii ndio itawezesha bei ya mbolea kuwa nafuu kwa kipindi kirefu kwa manufaa ya wakulima.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Wakenya wasisubiri muujiza kutoka kwa...

Teddy Mwambire achaguliwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi

T L