CHARLES WASONGA: Darubini kwa Chebukati uchaguzi wa 2022 ukinukia

CHARLES WASONGA: Darubini kwa Chebukati uchaguzi wa 2022 ukinukia

Na CHARLES WASONGA

HUKU ikiwa imesalia miezi 11 kabla ya Wakenya kuelekea debeni kuwachagua viongozi wapya, macho yote yanaelekezwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na hasa kinara wake Wafula Chebukati.

Hii ni kwa sababu tume hii ndio imetwika wajibu mkubwa wa kufanya maandalizi na hatimaye kuendesha uchaguzi huo Agosti 9, 2022.

Ili tume hii iweze kufanikiwa katika kazi hii muhimu, bila shaka inahitaji imani ya wadau kama vile vyama vya kisiasa, wagombeaji viti mbalimbali na Wakenya kwa ujumla.

Lakini kuaminiwa huku kutatokana na utendakazi mzuri wa tume hii inayoongozwa na Bw Wafula Chebukati.Ama kwa hakika, tangu kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017 na marudio ya uchaguzi wa urais mnamo Oktoba 26, mwaka huo, tume hii imeendesha chaguzi nyingi ndogo kwa njia ya kuridhisha.

Hii ni licha ya kujiuzulu kwa makamishna wanne na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji Bw Ezra Chiloba. Hii ndio maana sikubaliani na wanasiasa wa ODM ambao wameanzisha kampeni ya kutaka Bw Chebukati aondolewe mamlakani kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Nahisi kile mwenyekiti wa ODM John Mbadi, na wenzake, walioanzisha kampeni hiyo wiki jana wanapaswa kufanya ni kuisaidia IEBC katika maandalizi ya uchaguzi mkuu.

Ikizingatiwa kuwa muda uliosalia kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo ni mdogo, huu sio wakati wa kumfuta kazi mwenyekiti wa tume hii, bali kupiga jeki maandalizi ya tume hiyo kwa ajili ya zoezi hilo.

Kama mojawapo ya vyama vikuu vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo, ODM haina budi kuisaidia IEBC kufanikisha majukumu yake.

Kwa mfano, chama hiki kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila ODM, kupitia wabunge wake, kihakikishe IEBC imepewa fedha za kutosha za kuendesha shughuli zake.

Isitoshe, kupitia Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) na Kamati ya Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC), ni wajibu wa wabunge wa ODM kuhakikisha pesa zilizotengewa IEBC kufadhili maandalizi ya uchaguzi mkuu hazifujwi.

Huu wimbo ambao umeanzishwa na Bw Mbadi na wenzake kutaka Bw Chebukati ang’atuliwe hauna maana yoyote.Una madhara makubwa kwa sababu huenda ukatachangia wafuasi wa ODM na Wakenya wengine, kukosa imani na IEBC wakati muhimu kama huu.

Ukosefu wa imani kwa tume ni kutokubalika kwa matokeo ambayo itatangaza mwaka ujao haswa katika kinyang’anyiro cha urais, hali ambayo huenda ikasababisha fujo.

Kenya imewahi kuathiriwa na ghasia haswa baada ya chaguzi kuu za 2007 na 2017, kutokana na matamshi sawa na yale yaliyotolewa na wanasiasa wa ODM wiki jana.

Bw Mbadi na wenzake, wakome kabisa kushambulia IEBC hadharani walivyofanya wiki jana Homa Bay, wasije wakatumbukiza taifa hili katika lindi la machafuko tena.

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Viongozi waungane, ndio, lakini wasigawanye...

Dalili Kingi atafuta makao mapya OKA