CHARLES WASONGA: IEBC, CA wakome malumbano ili kufanikisha upeperushaji wa matokeo

CHARLES WASONGA: IEBC, CA wakome malumbano ili kufanikisha upeperushaji wa matokeo

NA CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi (IEBC) inahitajika kufanya kazi sako kwa bako na asasi nyingine husika za serikali ili iweze kuendesha uchaguzi mkuu ujao kwa njia huru, haki na yenye uwazi.

Mbali na hayo, tume hiyo inayoongozwa na Bw Wafula Chebukati inafaa kushauriana kila mara na vyama vya kisiasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo wa Agosti 9.

Hiyo ndiyo itakayojenga imani ya wawaniaji kwa utendakazi wa IEBC na kuchangia ukubalifu wa matokeo ya uchaguzi kuanzia ngazi ya udiwani hadi urais.

Kwa mantiki hii, malumbano yanayoendelea sasa kati ya IEBC na Halmashauri ya Mawasiliano nchini (CA) kuhusiana na suala muhimu la mtandao wa 3G hayafai.

Yanaweza kuchangia ghasia nchini endapo utata utatokea kuhusiana na matokeo ya uchaguzi wa urais kama iliyofanyika mnamo 2007.

Isitoshe, hali hii inaweza kutoa sababu za kufutiliwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais ilivyofanyika 2017. Juzi Mkurugenzi Mkuu wa CA, Bw Ezra Chiloba alisema asilimia 98 ya taifa la Kenya inafikiwa na 3G, ambayo IEBC itategemea kuwasilisha matokeo ya uchaguzi wa urais kutoka vituo vya kupigia kura hadi makao makuu ya kujumuisha kura jijini Nairobi.

Ila kamishna wa IEBC, Abdi Guliye amepinga kauli hiyo akisema si sahihi kwani sehemu nyingi hazijaunganishwa na mtandao wa 3G.

Anailaumu CA kwa kutoa habari za kupotosha “ilhali haijatuma maafisa wake kote nchini kubaini ikiwa sehemu zote zinafikiwa na mtandao wa 3G.”

Kwa upande wake, Bw Chiloba anajibu kwa kusema kuwa ni wajibu wa IEBC kuelekeza maafisa wake katika vituo vyake vyote vya kupigia kura ili waweze kuviunganisha katika mtandao huo.

Lakini kulingana na ripoti iliyotayarishwa na CA mwezi Aprili, ilibainika kuwa jumla ya vituo 1,100 vya kupigia kura havijaunganishwa na mtandao wa 3G. Kuna jumla ya vituo 53,000 vya kupigia kura. nchini vilivyoidhinishwa na IEBC.

Ikiwa kufikia Agosti 9, 2022, siku ya uchaguzi, vituo hivyo 1,100 havitakuwa vimeunganishwa na mtandao wa 3G ina maana kuwa matokeo ya uchaguzi wa urais.

Hii ni licha ya kwamba sehemu ya 44 (4) ya sheri ya uchaguzi inasema kuwa sharti matokeo hayo yatumwe kieletroniki kutoka vituo vyote hadi kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura.

Itakumbukwa kwamba mojawapo ya sababu iliyochangia Mahakama ya Juu kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais 2017 ilikuwa kwamba matokeo kutoka vituo 11,000 hayakuwasilishwa kieletroniki kulingana na sheria hiyo.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Ruto achunge ulimi wake, sifa ya ukabila...

Korti yaamua kesi ya kuzuia Sonko iendelee hadi mwisho

T L