CHARLES WASONGA: IEBC ifafanue masuala tata mapema kuhusu uwezo wake wa kufaulisha uchaguzi huru

CHARLES WASONGA: IEBC ifafanue masuala tata mapema kuhusu uwezo wake wa kufaulisha uchaguzi huru

NA CHARLES WASONGA

INAVUNJA moyo kwamba huku zikiwa zimesalia siku 47 kabla ya Wakenya kuelekea debeni kuwachagua viongozi wapya, maswali yametanda kuhusu kiwango cha utayarifu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kusimamia shughuli hiyo.

Kwa mfano, mnamo Juni 17 tume hiyo ilikosa kuchapishwa sajili ya mwisho ya wapigakura licha ya kuahidi kufanya hivyo mapema mwezi huu wa Juni.

Ahadi hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi baada ya kukamilika kwa shughuli ya uidhinishaji wa wagombea urais.

Sajili hiyo imekuwa ikisafishwa na kampuni ya KPMG tangu mwezi wa Mei ili kuondoa majina ya wapigakura waliokufa, waliojiandikisha zaidi ya mara moja na wale waliojiandikisha kwa kutumia stakabadhi ghushi.

Kulingana na ripoti ya awali ya KPMG, jumla ya wapigakura 246,465 katika sajili ya sasa ni wafu, wapigakura 481,711 walijisajili zaidi ya mara moja na wengine 226,143 walijisali kwa kutumia vitambulisho vya kitaifa visivyo vyao.

Aidha, inavunja moyo kwamba kufikia sasa IEBC haijajibu madai ya Naibu Rais William Ruto kwamba majina ya zaidi ya wapigakura 800,000 kutoka ngome zake yaliondolewa katika sajili ya wapigakura bila sababu maalum.

Isitoshe, tume hiyo haijatoa maelezo kuhusu madai ya baadhi ya wapigakura kwamba majina yao yalihamishwa, bila idhini yao, kutoka vituo walivyojiandikishia hadi vingine.

Suala jingine ambalo linawatia wadau, na Wakenya, wasiwasi ni kufikia sasa kuna jumla ya vituo 1,200 ambavyo havina mtandao wa 3G na 4G wa kufanikisha upeperushaji wa matokeo ya urais.

Hii ina maana kuwa matokeo kutoka vituo hivi huenda hayatawasilishwa kwa njia ya kielektroniki jinsi inavyohitajika kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, 2016.

Uhalali wa simu maalum, ambazo IEBC imetangaza zitatumika kuwasilishia matokeo ya uchaguzi kutoka vituo hivyo hadi kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura za urais, ni wa kutiliwa shaka.

Hii ni kwa sababu mojawapo ya sababu zilizopelekea Mahakama ya Juu kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais 2017, ni kwamba matokeo ya urais kutoka jumla ya vituo 11,000 hayakuwasilishwa kielektroniki.

IEBC iwahakikishie Wakenya kwamba hali kama hii haitatokea tena.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: IEBC haijatoa ripoti kuhusu madai ya...

KINYANG’ANYIRO 2022: Kaunti ya Kajiado

T L