CHARLES WASONGA: IEBC itoe maelezo muhimu kuhusu kura mara kwa mara

CHARLES WASONGA: IEBC itoe maelezo muhimu kuhusu kura mara kwa mara

NA CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inapokutana na wagombeaji urais wanne kesho Jumatano kujadili masuala muhimu kuhusu uchaguzi mkuu ujao, imefeli katika utoaji wa taarifa kila wakati kwa wanahabari kuhusu masuala muhimu kuhusu uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Ingawa wanahabari ndio wanaotegemewa pakubwa na wananchi kupata habari kuhusu maaandalizi ya shughuli hiyo muhimu ya kitaifa, imekuwa vigumu kwa wanahabari kupata ufafanuzi kutoka kwa wakuu wa tume hii kuhusu masuala yenye utata kuhusu maandalizi ya uchaguzi.

Kwa mfano, tangu mgombea urais wa chama cha UDA, Naibu Rais Dkt William Ruto kudai kuwa majina ya zaidi ya wapiga kura milioni moja anaoamini ni wafuasi wake yameondolewa kwenye sajili ya wapigakura, IEBC haijaeleza ni jinsi gani mgombeaji huyo wa urais alivyopata habari hizo.

Alitoa madai hayo mbele ya mabalozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) ambao umekuwa ukiwatuma waangalizi kufuatilia chaguzi nchini katika miaka ya nyuma.

Mwenyekiti wa tume hiii, Bw Wafula Chebukati hajaelezea wanahabari ni vipi Dkt Ruto alivyojua majina yaliyoondolewa kutoka sajili ya wapiga kura ni ya wafuasi wake pekee.

Bw Chebukati hajaeleza ni vipi Dkt Ruto alivyofaulu kupata habari hizo na wala sio washindani wake; Raila Odinga wa Azimio la Umoja One-Kenya, Prof George Luchiri Wajackoyah (chama cha Roots) na David Mwaure Waihiga wa Agano.

Isitoshe, mwenyekiti huyo hajaeleza ikiwa majina hayo yalirejeshwa miongoni mwa majina 22, 120, 458 ya wapigakura yaliyoko kwenye sajili rasmi iliyochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali Jumatano wiki jana.

Suala kama hili ni lenye uzito zaidi ikizingatiwa kuwa liliibuliwa katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mnamo 2017.

Inasikitisha kuwa huku zikisalia siku 41 kabla ya Wakenya kuelekea debeni kuwachagua viongozi wapya, IEBC ingali inavutana na wadau mbalimbali kuhusu sajili ya wapigakura.

Imeshikilia kwamba ni sajili ya kidijitali pekee itakayotumika kuwatambua wapigakura na wala sio sajili ya daftari ambayo imekuwa ikitumika kama mfumo mbadala katika vituo vya kupigia kura ikiwa mitambo ya kielektroniki (KIEMS) itafeli kufanya kazi.

Tume hii haijatoa maelezo kamili kwa wanahabari, ambao wataupitisha kwa wapigakura, kuhusu mikakati ambayo imewekwa kuzuia visa vya kufeli kwa mitambo hiyo siku ya uchaguzi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan, majuzi alisema kuwa tume hiyo ilifikia uamuzi huo ili kuzuia mwanya ambao umekuwa ukitumiwa na baadhi ya maafisa wasimamizi wa uchaguzi kuendeleza hila kwa “kupiga kura kwa niaba ya wapiga kura ambao hawatajitokeza”.

Japo, kauli hii ina mantiki fulani, Bw Marjan hajaelezea ni vipi, kwa mfano, wapiga kura ambao hawataweza kutambuliwa kidijitali kupitia alama za vidole vyao watakavyoruhusiwa kupiga kura.

Hajaeleza waziwazi mikakati ambayo tume hiyo imeweka kuhakikisha kuwa kutakuwa na mitambo ya ziada ambazo zitatumika endapo ile ya awali itafeli.

Wapiga kura ambao ndio wadau wakuu katika uchaguzi huu wa Agosti 9, wanafaa kupata hakikisho kwamba hawatazuiwa kupiga kura endapo mitambo ya KIEMs itafeli.

IEBC inafaa kutoa maelezo kuhusu suala hilo kwa wapiga kura mapema kando na kudai kuwa “watu wote wenye vitambulisho vya kitaifa au paspoti wataruhusiwa kupiga kura.”

  • Tags

You can share this post!

Mwigizaji Michelle Wanjiku apania kufuata nyayo zake Lupita...

BENSON MATHEKA: Serikali isake magenge yote hatari kote...

T L