CHARLES WASONGA: KEMSA yadai wafanyakazi wa chini wasifutwe kazi

CHARLES WASONGA: KEMSA yadai wafanyakazi wa chini wasifutwe kazi

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA) kuwatuma jumla ya wafanyakazi 600 kwa likizo ya lazima ikijiandaa kuwafuta kazi ni haramu na inakiuka haki za kibinadamu.

Madai ya mwenyekiti wa bodi ya mamlaka hiyo, Bi Chao Mwadime kwamba hiyo ni sehemu ya mpango wa mageuzi katika asasi hiyo iliyozongwa na sakata ya ufisadi mwaka jana, hayana mashiko.Si haki kwa Kemsa kuwapiga kalamu wafanyakazi wa ngazi za chini kwa sababu ya maovu yaliyotekelezwa na maafisa wa ngazi za juu ambao walisimamishwa kazi mwaka jana.

Kinaya ni kwamba wakuu hao waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za kushiriki katika wizi wa Sh7.8 bilioni kupitia ununuzi wa vifaa vya kupambana na corona, wangali wanapokea nusu ya mishahara yao.

Wao ni aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji, Bw Jonah Manjari aliyesimamishwa kazi kwa muda, kwa kukiuka sheria wakati wa utoaji wa zabuni za ununuzi wa bidhaa kama vile barakoa na vifaa kinga (PPEs).Wengine ni aliyekuwa mkurugenzi wa Idara ya Ununuzi, Bw Charles Juma na aliyekuwa mkurugenzi wa Huduma za Kibiashara, Bw Eliud Mureithi.

Isitoshe, hivi majuzi, aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya Kemsa, Bw Kembi Gitura alitajwa katika ripoti ya kamati ya bunge la kitaifa kuhusu uwekezaji (PIC), kama mmoja wa walioshawishi utoaji wa zabuni hizo kinyume cha sheria.

Inashangaza kwamba baada ya maafisa wakuu wa Kemsa kusimamishwa kazi Agosti mwaka jana ili kutoa nafasi kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu sakata hiyo, Bw Gitura alihamishwa hadi Tume ya Mawasiliano Nchini (CA) kushikilia wadhifa huo huo wa mwenyekiti wa bodi.

Kamati hiyo ya PIC, inayoongozwa na Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Sherrif Nassir, ni moja kati ya asasi zilizochunguza sakata hiyo iliyofichuliwa Juni mwaka jana.Bi Mwadime na wanachama wa bodi hii mpya ya Kemsa, hawafai kuanza kutekeleza mageuzi katika asasi hii kwa kuwafuta kazi wafanyakazi wa ngazi za chini.

Ama kwa kweli wafanyakazi hawa hawakuhusika moja kwa moja katika ufisadi uliozonga taasisi hiyo mwaka jana.Serikali Kuu, kupitia Wizara ya Afya ingeanza mchakato wa kuleta mageuzi kama Kemsa kwa kuwaadhibu maafisa wakuu waliohusika katika sakata hiyo iliyochangia wizi wa pesa za umma.

Wakurugenzi wa kampuni zilizoshiriki katika wizi huo wa mabilioni ya pesa za umma wakati wa janga la corona pia wanafaa kufunguliwa mashtaka.Hatua dhidi ya wafanyakazi 600 wa ngazi za chini kunaonyesha kuwa kuna njama ya kuharibu ushahidi ambao ulipasa kutumiwa kuwahukumu maafisa wakuu wa Kemsa ambao ni watuhumiwa wa sakata hiyo.

Swali langu ni je, mbona kamati za afya katika bunge la kitaifa na seneti, Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathugu na EACC zilizochunguza sakata hiyo, hazikupendekeza kufutwa kwa wafanyakazi?

Mbona mpaka sasa maafisa wa Kemsa na watu wengine waliotajwa katika ripoti za chunguzi hizo hawajashtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi hii?Wabunge na Maseneta wapinge kabisa mpango huu wa kuwafuta kazi “samaki wadogo” huku “mapapa” waliomeza pesa za umma wakisazwa.

You can share this post!

WANTO WARUI: Wanafunzi wafunzwe kuwa demokrasia ina mipaka

Hofu hali ya kiangazi kuibua janga jipya

T L